MABINGWA wapya wa Kagame timu ya soka ya Yanga, wamesema chini ya uongozi uliopo wataendelea kuwafunga mahasimu wao wa jadi, Simba pindi watakapokutana.
Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga (pichani)alisema hivi karibuni kuwa uwepo wao Yanga ni kwa ajili ya maendeleo ya Yanga na si kimaslahi na ndiyo maana timu imeweza kupata mafanikio chini yao.
Alisema, wameweka mikakati ya kuhakikisha wanakuwa na kikosi na kocha bora ambacho kwa namna moja amba nyingine kitakuwa kinafanya mambo makubwa hali ambayo imedhihirika.
“Ushindi wa timu yetu ni mikakati tuliyojiwekea viongozi, hii haitaishia hapa kwani tumepanga kufanya mambo makubwa zaidi ili kudhihirisha kuwa tulisaka uongozi kwa ajili ya kurejesha heshima ya Yanga,”Alisema Nchunga.
Chini ya uongozi wa Nchunga, Yanga imekutana na Simba mara tano na kushinda mara tatu, sare mara moja na kufungwa mara moja, ambapo katika Ngao ya hisani Yanga ilishinda kwa penati,huku meshi ya mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ilishinda 1-0, kabla ya kufungwa mabao 2-0 kwenye kombe la mapinduzi na baadaaye 1-1, huku juzi ikishinda bao 1-0.