Usajili wa wachezaji wenye umri chini ya miaka kumi na saba kwa ajili ya michuano ya Airtel Rising Stars, ambao ni mpango wa kukuza vipaji vya wachezaji wa mpira wa miguu kuanzia ngazi ya chini hadi ya taifa, unaanza leo. Mpango huo ambao unadhaminiwa na Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kwa kushirikiana na klabu ya Manchester United ya Uingereza, utafanyika kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Morogoro.
Akizungumzia michuano hiyo ya Airtel Rising Stars, Mkurungenzi wa Masoko wa Airtel Tanzania Cheikh Sarr, alisema kampuni yake inajivunia kukuza vipaji vya vijana na kwamba huu ndio muda ambao watu wengi walikuwa wanaousubiri. ‘Huu ndio muda muafaka wa kutengeneza wachezaji nyota wa mpira wa miguu kutoka hapa nchini’, aliongeza Bw. Cheikh.
Michuano hiyo ngazi ya mkoa inatarajiwa kuanza Jumapili tarehe 17 Julai ambapo kwa mkoa wa Dar es Salaam utawakilishwa na timu 12 kutoka katika wilaya za Kinondoni, Temeke na Ilala wakati mikoa ya Morogoro, Mwanza na Arusha itaingiza timu nne kila moja.
Mechi zote za mikoani zinatarajiwa kumalizika Jumamosi ya tarehe 30 Julai ambapo kila mkoa utatoa timu moja ambayo itaungana na timu kutoka mikoa mingine kwenye michuano ya fainali itakayochezwa jijini Dar es Salaam mwezi Septemba mwaka huu. Wachezaji sita bora kwenye fainali hio watachanguliwa kuungana na wachezaji kutoka nchi zingine za Afrika kwenye kambi maalumu ambayo itafanyika chini ya usimamizi wa walimu kutoka katika klabu ya Manchester United na kufanyika hapa nchini Tanzania.
Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Tanzania (TFF) watakuwa na mkutano na waandishi wa habari Alhmisi ya tarehe 14 Julai, kwa ajili ya kutoa maelezo zaidi juu ya Airtel Rising Stars.
Airtel Rising Stars ni mpango kambambe wa Afrika nzima ambao utakuwa ni wa kutafuta na kukuza vipaji vya soka vinavyochipukia kwa wavulana na wasichana wenye miaka chini ya kumi na saba ambao watapata muda muafaka wa kuonyesha vipaji vyao na kukutana na waatalum wa mpira wa miguu ambao watawapa mafunzo zaidi na kupata nafasi ya kukuza vipaji vyao.
Airtel Rising Stars ilizinduliwa rasmi katika shule ya Sekondari ya Makongo tarehe 29 Juni mwaka huu na Mshambuliaji wa zamani wa timu ya Manchester United Andy Cole. Andy Cole pia ni mchezaji wa zamani wa timu ya Uingereza na alicheza miaka saba kwenye klabu ya Manchester United na alikuwa kwenye kikosi kilichoshinda medali tano kati ya 19 ambazo Man U imeweza kushinda mpaka sasa.
Akizungumzia kuhusu mpango wa Airtel Rising Stars, Cole alisema kwamba anayo furaha kushiriki mpango huu wa kutafuta vipaji vya vijana kwa hapa Tanzania na Afrika kwa ujumla na yuko tayari kuwapa ujuzi na mbinu zaidi juu ya mpira wa miguu.