YANGA KUTOSHIRIKI TENA MICHUANO YA KAGAME

NA DINA ISMAIL
MABINGWA wapya wa michuano ya klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati - Kagame Castle Cup 2011, Yanga, wameapa kamwe hawatacheza tena michuano hiyo hadi zake, hasa ya mgawanyo wa mapato zitakaporekebishwa.
Msimamo huo mgumu umetolewa jana na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga (pichani)ikiwa ni siku tatu tangu timu hiyo itwae ubingwa wa michuano hiyo kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba.
Bao hilo pekee katika mechi ya fainali iliyochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, lilipachikwa nyavuni dakika ya 108 na mshambuliaji wake wa kimataifa, Mghana Keneth Asamoah.
Nchunga ambaye ni mwanasheria kitaaluma, aliieleza Sayari kuwa kwa kanuni zilizopo za michuano hiyo, ni wazi klabu zinanyonywa kupita kiasi, hivyo wao Yanga hawatashiriki tena hadi marekebisho yafanyike.
“Hatuna tatizo na michuano hii, isipokuwa ipo haja sasa kwa wahusika (Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati - Cecafa), kufanya mabadiliko ya kanuni hasa mgawanyo wa mapato,” alisema Nchunga.
Nchunga aliyeingia madarakani Julai 18, mwaka jana, alisema Yanga haitakuwa tayari kushiriki hadi pale suala la mgawo wa mapato ya mechi za michuano hiyo litakapokuwa wazi na kuzinufaisha klabu.
Akizungumza kwa masikitiko makubwa jana, alisema kuendelea kushiriki michuano hiyo chini ya kanuni za sasa, ni klabu kukubali kunyonywa huku fedha hizo zikiwanufaisha wengine.
Nchunga alisema, kilichowasikitisha ni kuambulia kiasi cha sh mil 16 tu za mgawo wa mechi ya fainali iliyopigwa Jumapili na kuingiza kiasi cha shilingi mil. 354.5.
“Hivi kwa unyonyaji wa aina hii, klabu zitapiga hatua ya kiuchumi kweli chini ya mwamvuli huu wa Cecafa? Hapana, hatuwezi kushiriki michuano hii tena hadi pale kanuni zitakapofanyiwa marekebisho,” alisisitiza Nchunga.
Alisema kwa mgawanyo wa sasa wa mapato ya mechi za michuano hiyo, klabu ndizo zinaumia kutokana na kutumia gharama kubwa kuandaa timu na fedha zinazopatikana hazifiki hata nusu.
“Kwa hali hii, mwakani hatutakuwa tayari kushiriki michuano hii, lazima tukae kwanza na viongozi wa CECAFA kuboresha kanuni, hasa mgawanyo wa mapato,”alisema Nchunga.
Si mara ya kwanza Yanga kulalamikia mgawanyo wa mapato ya michuano hiyo. Mwaka 2008, iligomea kucheza na Simba katika mechi ya kuwania mshindi wa tatu ikitaka kupewa sh mil 50 kwanza.
Licha ya kuwepo kwa madai ya Simba na Yanga kukubaliana kutoingiza timu hadi kila moja ipewe kiasi hicho, watani zao waliingiza timu, hivyo wao kufungiwa miaka mitatu na kulimwa faini ya dola 30,000.
Aprili mwaka huu, Yanga waliomba radhi kwa kosa hilo na kuomba wapunguziwe faini, hivyo wakarejeshwa na kutakiwa kulipa dola 20,000 za Marekani.
Wakirejea kwenye michuano hiyo wakitoka kifungoni, Yanga wamefanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa kuwafunga Simba, hivyo kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa huo mara nne tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo mwaka 1974.
Kabla ya Jumapili, Yanga imewahi kutwaa ubingwa wa michuano hiyo mwaka 1975, 1993 na 1999.  
Aidha, Nchunga alisema pamoja na hayo, uongozi umewapa wachezaji na viongozi wa timu hiyo dola 15,000 za Marekani ambazo ni nusu ya zawadi ya ubingwa. 
Alisema, mbali ya kiasi hicho, pia baadhi ya wadau, marafiki na wakereketwa wa Yanga, wameahidi kutoa zawadi ya fedha kwa wachezaji kiasi cha sh mil 20.

Post a Comment

Previous Post Next Post