ELECTIONS COMMITTEE
TAARIFA
KWA VYOMBO YA HABARI
06 MACHI 2012
UFAFANUZI KUHUSU MAJUKUMU, WAJIBU NA MAMLAKA
YA KAMATI YA UCHAGUZI NA MAELEZO YA KINA KUHUSU MAAMUZI
YA KAMATI ZA UCHAGUZI ZA TFF KUHUSU MAOMBI YA NDG. MICHAEL RICHARD WAMBURA KUGOMBEA UONGOZI KWENYE UCHAGUZI WATFF 2008, UCHAGUZI WA KLABU YA SIMBA 2010 NA
FAM 2011.
1. USIMAMIZI WA CHAGUZI ZA
WANACHAMA WA TFF
Muundo wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) umeelezwa wazi kwenye Katiba ya TFF
Ibara ya 18. Kamati ya Uchaguzi ya TFF ni moja kati ya vyombo sita vilivyoainishwa
katika Muundo wa TFF. Majukumu, wajibu na mamlaka ya vyombo vya TFF yameainishwa
katika Katiba ya TFF na Kanuni zilizotungwa na kuidhinishwa na Kamati ya
Utendaji ya TFF kwa kuzingatia Ibara ya 34 ya Katiba hiyo.
Majukumu, wajibu na mamlaka ya
Kamati ya Uchaguzi ya TFF yameainishwa kwenye Katiba ya TFF Ibara ya 49 na
kwenye Kanuni za Uchaguzi za TFF na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF.
Mbali na majukumu na wajibu wa kusimamia uchaguzi wa TFF na chaguzi za wanachama
wake na kuishauri Kamati ya Utendaji ya TFF kuhusu Kanuni za Uchaguzi, Kamati ya
Uchaguzi ya TFF inao wajibu wa kulinda Katiba na Kanuni za uchaguzi za TFF na
Katiba ya FIFA na Katiba za wanachama wa TFF kama ilivyotamkwa kwenye Kanuni za
Uchaguzi za TFF Ibara ya 6 na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya
26. Uchaguzi
Mkuu wa TFF hufanyika kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa TFF. Chaguzi za
wanachama wa TFF na wanachama wao hufanyika kwa mujibu wa Kanuni za uchaguzi za
wanachama wa TFF na si vinginevyo. Kanuni hizi zimeainisha taratibu mbalimbali
ambazo lazima zizingatiwe kikamilifu, ikiwa ni pamoja na utaratibu wa ukataji
rufaa katika ngazi mbalimbali za uchaguzi. Vyombo na Kamati zote za
TFF, Wanachama wote wa TFF na wanachama wao, na wadau wote wa soka wanao
wajibu wa kuheshimu Kanuni mbali mbali za TFF ambazo ni pamoja na Kanuni za
Uchaguzi.
2. MAAMUZI KUHUSU MAOMBI YA
UONGOZI YA NDG. MICHAEL WAMBURA
Kwa muda mrefu pamekuwepo na
taarifa mbalimbali kupitia vyombo vya habari zenye lengo la kuwafanya wadau na
wapenzi wa soka na umma wa watanzania kwa ujumla kuaminishwa kuwa Ndg. Michael
Wambura huonewa na vyombo vya TFF vinavyosimamia uchaguzi kila anapoomba nafasi
za uongozi katika TFF. Baadhi ya vyombo vya habari na baadhi ya wapenzi wa soka
wamesikika wakisema kwamba kuenguliwa kwa Ndg. Michael Wambura kugombea uomgozi
ni kutokana na kuogopwa na viongozi wa TFF. Kamati ya Uchaguzi ya TFF inapenda
kufafanua kwa kina maamuzi yote yaliyofanyika kuhusu maombi yote ya uongozi ya
Ndg. Michael Wambura na kuweka wazi vielelezo vilivyotumika kufikia maamuzi hayo
ili umma wa watanzania wafahamu kinagaubaga ukweli kuhusu maamuzi
hayo:
UCHAGUZI MKUU WA TFF
2008
Kamati ya Uchaguzi ya TFF
ilimwengua Ndg. Michael Wambura kugombea nafasi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa
TFF kwa kutokidhi matakwa ya uadilifu kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi na Katiba
ya TFF. Ndg. Michael Wambura hakuridhika na uamuzi huo na alikata rufaa kwenye
Kamati ya Rufaa ya TFF. Hata hivyo baada ya Kamati ya Rufaa kupitia nyaraka
mbali mbali zilizowasilishwa kwenye Kamati hiyo ikiwa ni pamoja na ripoti ya
ukaguzi wa maheabu ya TFF/FAT kwa mwaka 2002, 2003 na 2004 rufaa yake ilishindwa
baada ya Kamati ya Rufaa kuridhika na kuweka bayana kuwa mwomba rufaa, Michael
Richard Wambura aliipa Zabuni kampuni yake iitwayo Min Investments &
Commercial Services Co. wakati akiwa Katibu Mkuu wa FAT/TFF na hivyo
kushindwa kukudhi kigezo cha uadilifu. Katika kufikia maamuzi yake,
Kamati ya rufaa pia ilibaini kuwa Ndg. Michael Richard Wambura alionyesha kuwa
alikuwa amechana na umiliki wa kampuni hiyo kuanzia tarehe 12 Novemba 2003 kwa
mabadiliko yaliyotekelezwa tarehe 28 Februari 2007 kwa malipo ya Shs. 34,500/=
ya “exchequer receipt No. 28173444’. Hata hivyo, Kamati ya Rufaa
iliridhika kuwa utekelezaji wa mabadiliko ya umiliki wa kampuni hiyo ulichukua
takribani miezi arobaini (40). Baada ya majadiliano ambayo yalikuwa yamekitwa
(pegged) kwenye uadilifu (integrity), Kamati ya Rufaa iliridhika kuwa
taswira inayojitokeza kwenye muktadha imegubikwa na wingu jeusi la mashaka
kuhusu “integrity” ya Muomba Rufaa (Ndg. Michael Richard
Wambura).
Uthibitisho kwamba mmilki wa
Kampuni ya Min Investments & Commercial Services Co ni Ndg.
Michael Richard Wambura ulitolewa na Msajili wa Makampuni (Business Registration
and Licensing Agency-BRELA) kwa barua yenye Kumbukumbu Na. MITM/RBN/93017 ya
tarehe 16 Agosti 2006. Kampuni hiyo ilisajiliwa tarehe 17 Julai
1992.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF
inatoa sehemu ndogo tu ya ubadhirifu uliokuwa unafanywa kwa kutumia Kampuni hiyo
(Min Investments & Commercial Services Co) ya Michael Wambura kinyume
na utaratibu wa utoaji tenda wa FAT/TFF na malipo aliyojilipa bila maelezo
yoyote kama ilivyoainishwa kwenye Ripoti ya Ukaguzi wa Mahesabu iliyowasilishwa
na wakaguzi tarehe 19 Septemba 2005 na Ripoti maalumu ya ukaguzi iliyowasilishwa
Novemba 2006, kama ifuatavyo:
(i) Tarehe 28 Julai 2004 Michael
Wambura akiwa Katibu Mkuu wa TFF alilipwa Dola za Kimarekani 16,548.00 (US$
16,548 sawa na Tshs. 17,170,040 wakati huo) kwa ununuzi wa samani (furniture) za
Hosteli ya TFF. Pesa hizo zilizoombwa kulipwa kwa Michael Wambura zimeonyeshwa
kwenye fomu ya malipo ya TFF ya tarehe 28 Julai 2004. Pesa hizo zilipokelewa na
Kampuni ya Min Investments & Commercial Services Co na kuthibitisha
kupokelewa na kampuni hiyo kwa risiti Na. 020 ya tarehe 21 Julai 2004 ya kampuni
hiyo, ingawa hapakuwa na maombi ya manunuzi (order) iliyokuwa imefanywa na TFF
kwa kampuni hiyo.
(ii) Baada ya kujilipa pesa
zilizotajwa hapo juu, kesho yake tarehe 29 Julai 2004 Ndg. Michael Wambura akiwa
Katibu Mkuu wa TFF alijilipa Dola za kimarekani 25,000.00 (US$ 25,000.00 sawa na
Tshs. 25,937,500 wakati huo), kama ilivyoonyeshwa kwenye vocha ya malipo ya TFF
Na. 5324 ya tarehe tajwa hapo juu, ikionyesha kuwa ni kwa ajili ya malipo ya
samani za Hosteli (US$ 15,000.00) na malipo ya awali ya Gari (US$ 10,000.00).
Ndg. Michael Wambura alithibitisha kupokea malipo hayo. Ripoti ya Ukaguzi
inabainisha wazi kuwa vifaa vichache vilivyonuliwa kwa hosteli ya TFF thamani
yake haikuainishwa na hapakuwa na gari lililolipiwa malipo ya awali katika
vitabu vya mahesabu ya TFF.
(iii) Katika kipindi cha mwaka 2002
Ndg. Michael Wambura akiwa Katibu Mkuu wa FAT alijikopesha jumla ya Tshs.
36,850,750 bila idhini ya Kamati ya Utendaji.
(iv) Tarehe 20 Mei 2002 Ndg.
Michael Wambura akiwa Katibu Mkuu wa FAT alijilipa Tshs. 12,147,837 ambazo
hazina maelezo yoyote.
(v) Imebainishwa wazi kuwa
FAT/TFF ilikuwa mfilisi katika kipindi cha 2002-2004 (Nukuu: “The Association
was actually insolvent during the period.”)
Kamati inaweka wazi tena
kwamba maamuzi yaliyofikiwa na Kamati ya Rufaa ya kumuengua Michael Wambura
kwenye uchaguzi Mkuu wa TFF yanaweza tu kubadilishwa na Mahakama ya usuluhishi
wa masuala ya michezo (CAS) endapo Michael Wambura atakata rufaa CAS kupinga
maamuzi hayo na kushinda rufaa, na si vinginevyo.
MAAMUZI YA MKUTANO MKUU WA
TFF 2007
Mkutano Mkuu wa
TFF ambacho ndicho chombo cha juu kabisa cha TFF (Supreme Authority of
TFF) katika kikao chake mwaka 2007 kilipitia ripoti za ukaguzi wa mahesabu
ya FAT/TFF kwa kipindi cha mwaka 2002 hadi 2004 na baada ya kujiridhisha kuhusu
ubadhirifu uliofanywa na Ndg. Michael Wambura, Mkutano Muu wa TFF uliamua kwamba
Ndg. Michael
Wambura afikishwe kwenye vyombo vya dola kwa ubadhirifu wa fedha za FAT/TFF
alioufanya kama ilivyoainishwa kwenye ripoti za ukaguzi wa Mahesabu.
Sekretarieti ya TFF mwaka 2007 ikitekeleza maagizo ya Mkutano Mkuu wa TFF na
suala hilo lilpelekwa Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi ilithibitisha maombi ya
TFF kwa barua yake ya tarehe 18 Januari 2008 na kumfungulia jalada
Ndg Michael Wambura kwa kosa la wizi akiwa Mtumishi.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF inaheshimu maamuzi ya Mkutano Mkuu wa TFF na hadi sasa
haijataarifiwa kwa maandishi na chombo chochote kama suala hilo limefikia ukomo
wa aina yoyote.
UCHAGUZI WA KLABU YA SIMBA
MWAKA 2010
Ndg. Michael Richard Wambura
aliomba kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Klabu ya Simba. Hata hivyo alikatiwa
rufaa na Ndg. Daniel T. Kamna kwa kutotimiza matakwa ya Ibara ya 9
ya Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF kama ilivyoamuliwa na Kamati ya
Uchaguzi ya TFF na pia Kamati ya Rufaa ya TFF mwaka 2008 wakati alipoomba
kugombea nafasi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa TFF. Kamati ilikubaliana na
maamuzi yaliyotolewa na Kamati ya Uchaguzi na Kamati ya Rufaa ya TFF mwaka 2008
kwamba Bw. Michael R. Wambura si mwadilifu kama
ilivyonyeshwa kwenye aya ya 2.1 na 2.2 hapo juu na hivyo hakukidhi matakwa ya
Ibara ya 29(7) ya Katiba ya TFF na Ibara ya 9 ya Kanuni za Uchaguzi za wanachama
wa TFF. Kamati ilimuondoa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Simba
SC.
Baada ya maamuzi hayo ya
Kamati, Ndg. Michael Richard Wambura alikwenda Mahakamani na akafungua kesi
kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es salaam dhidi ya Mwenyekiti wa
Klabu ya Simba kuzuia uchaguzi wa klabu ya Simba usifanyike. Kwa kufanya hivyo
alivunja Katiba ya Klabu ya Simba na kukiuka Katiba ya TFF Ibara ya 12(2) (e) na
Katiba ya FIFA Ibara ya 64(2). Klabu ya Simba ilichukua hatua za kikatiba, na
katika kikao chake cha 5/5/2010, ilimsimamisha uanachama Ndg. Wambura kwa
kukiuka katiba ya klabu hiyo. Klabu ya Simba iliitaarifu TFF uamuzi huo kwa
barua yenye Kumbukumbu Na. SSC/MMKT/162/Vol.40/10 ya tarehe 06 Mei 2010
iliyoambatanishwa na Muhtasari wa kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanya
uamuzi huo. Uamuzi wa kumrudishia uanachama unafanywa na Mkutano Mkuu wa Klabu
ya Simba. TFF haijapokea taarifa yoyote kutoka Klabu ya Simba kwamba Mkutano
Mkuu wa Klabu hiyo ulikwisha msamehe. Kwa hali hiyo taarifa ya kusimamishwa
kwake iliyotumwa TFF mwezi Mei 2010 itaendelea kuzingatiwa hadi hapo Klabu ya
Simba itakapo ijulisha TFF mabadiliko ya maamuzi hayo.
3.
MAAMUZI KUHUSU UCHAGUZI WA
FAM
Kamati ya Uchaguzi ya TFF
ilimuondoa Ndg. Michael Wambura kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa FAM kwa kuwa
alifungua kesi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es salaam dhidi ya
Mwenyekiti wa Klabu ya Simba akiwa ni mwanachama wa Klabu ya Simba kuzuia
uchaguzi wa klabu ya Simba usifanyike, jambo ambalo ni uvunjaji wa Katiba ya
Klabu ya Simba, ukiukwaji wa Katiba ya FAM, TFF na FIFA.
Pia, Kamati ya Uchaguzi ya
TFF iliweka wazi kama ilivyobainisha kwenye uchaguzi wa Klabu ya Simba kwamba
suala la uadilifu wa Ndg. Wambura lilishafanyiwa maamuzi na Kamati ya Rufaa ya
TFF mwaka 2008 kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi Mkuu wa TFF. Kwa mujibu wa
Kanuni za Uchaguzi huo na Katiba ya TFF Mamlaka pekee inayoweza kutengua uamuzi
huo ni Mahakama ya Usuluhishi wa masuala ya Michezo (CAS) iliyo na makao yake
Lausanne , Switzerland .
Baada ya uamuzi huo, Kamati
ya Uchaguzi ya TFF imeshuhudia baadhi ya vyombo vya TFF vikishughulikia masuala
ya uchaguzi kinyume na matakwa ya Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi, kama
ifuatavyo:
(i) Katika hali isiyozingatia
Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF, Kamati ya Nidhamu ilipokea malalamiko ya
Ndg. Michael Wambura yaliyoitwa ‘rufaa’. Kwa kuwa hakuna utaratibu wa masuala ya
uchaguzi kukatiwa rufaa kwenye Kamati za nidhamu katika ngazi zote za uchaguzi
na hivyo pia kutokuwepo ada ya ‘rufaa’ za aina hiyo, mlalamikaji alilazimisha
kupokelewa ada ya Tshs 300,000/= ambayo ni ada inayotumika kwa rufaa za Ligi
Kuu ya Vodacom ambayo imeainishwa katika Ibara ya 17 ya kanuni za
mashindano hayo. Ada hiyo iliwekwa (deposited) kwenye Akaunti ya TFF bila ridhaa
ya TFF. Pamoja na mapungufu hayo “rufaa’ hiyo ilisikilizwa na Kamati ya Nidhamu
na kutolewa maamuzi. Mlalamikaji hakuridhika na maamuzi ya Kamati hiyo na
aliamua kukata ‘rufaa’ katika Kamati ya Rufaa ya TFF.
(ii) Kamati ya Rufaa ya TFF
ilipokea na kusikiliza ‘rufaa’ ya Ndg. Michael Richard Wambura, kinyume na
matakwa ya Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF. Kwa kuwa kwa mujibu wa Kanuni
za Uchaguzi za wanachama wa TFF hakuna rufaa inayokatwa kwenye Kamati hiyo,
hivyo kutokuwapo ada yoyote kwa “rufaa” ya aina hiyo, ili kutimiza azma ya
kusikiliza ‘rufaa’ hiyo, palifanyika juhudi za kulazimisha kupokelewa ‘ada’ ya
Shilingi 500,000/= ambayo ni ada ya rufaa za mashindano ya Ligi Kuu ya Vodacom
ambayo imeainishwa pia katika Ibara ya 17 ya kanuni za mashindano ya Ligi Kuu
ya Vodacom. Hata hivyo, ada hiyo ambayo si halali, haikupokelwa na
Sekretarieti ya TFF baada ya kushindikana kuainisha ada ya
mashindano ya Ligi Kuu ya Vodacom na masuala ya Uchaguzi. Bila
kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF na Katiba ya TFF Ibara ya
47(4) inayotamka na kuikataza Kamati ya Rufaa kusikiliza rufaa kwa
mambo yaliyowekewa ukomo na Kanuni husika; Ibara hiyo inatamka; ‘The Appeal
Committee shall be responsible for hearing appeals against decisions from the
Disciplinary Committee that are not declared final by relevant regulations as
well as decision passed by the players’ Status Committee concerning the
eligibility of players for the teams’, Kamati hiyo ilisikiliza malalamiko ya
Ndg. Michael Richard Wambura na kutoa uamuzi bila kuzingatia Kanuni za Uchaguzi
za wanachama wa TFF ambazo ni ‘relevant regulations’ na Ibara ya 12(4) ya Kanuni
hizo kutamka wazi kuwa; ‘The decisions of the TFF Elections
Committee are final and conclusive and shall not be monitored by any other
body’.
(iii) Kamati ya Uchaguzi ya TFF
inatamuka wazi kuwa utaratibu mzima uliotumika kupokea rufaa hiyo toka Kamati ya
Nidhamu hadi ya Kamati ya Rufaa haukufanyika kwa mujibu wa taratibu za ukataji
rufaa zilizoainishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF.
Ukataji rufaa huo uliongozwa zaidi na hila kuliko dhamira ya kuheshimu
taratibu zilizowekwa. Mbali na kutumia kanuni za Ligi kuu ya Vodacom kusikiliza
‘rufaa’ hizo, uthibitisho mwingine wa hila na ujanjaujanja ni pale mlalamikaji
alipokwenda kuweka kwenye akaunti ya TFF ada ya rufaa ya mashindano ya Ligi Kuu
ambayo haitambuliki kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi na kutumia vyombo vya
habari kutangaza kitendo hicho, lakini baada ya kutolewa maamuzi na Kamati ya
Rufaa alienda kimya kimya TFF kuchukua ada hiyo ambayo ni ya rufaa kwa
mashindano ya Ligi kuu.
(iv) Kamati ya Uchaguzi ya TFF,
kwa mamlaka yaliyo kasimiwa kwake na Katiba ya TFF Ibara ya 49(1) , Kanuni za
Uchaguzi za TFF Ibara ya 6, Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya
8(2), 10(6), 12(4) na 26(2), na pia kwa mamlaka yaliyoainishwa katika Katiba za
wanachama wa TFF kuhusu uchaguzi, katika kikao chake kilichofanyika 03 Desemba
2011 iliamua na inatamka wazi kuwa maamuzi yaliyofanywa na Kamati ya Rufaa ni
BATILI kwa kuwa hayakuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF. Kamati ya
Uchaguzi ya TFF inaziagiza Kamati zote za Uchaguzi za wanachama wa TFF na
wanachama wao kuendelea kuzingatia Kanuni za Uchaguzi katika utendaji wa kazi
zao za kuendesha na kusimamia chaguzi zote za vyama vya mpira wa miguu nchini,
ikiwa ni pamoja na kutozingatia maamuzi yoyote ya uchaguzi yatakayofanyika
kinyume na Kanuni za Uchaguzi.
4.
TAARIFA ZA UDANGANYIFU KUTOKA
KWA BAADHI YA WAGOMBEA UONGOZI KWENYE VYAMA WANACHAMA WA TFF.
Kamati ya Uchaguzi inapenda
kuwakumbusha wadau wote wa soka wenye nia ya kugombea uongozi TFF na vyama
wanachama wa TFF kuwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za TFF ibara ya 25(8) na
Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 26(8) ni makosa
kuwasilisha taarifa za udanganyifu kwenye Kamati ya Uchaguzi. Kanuni hizo
zinatamka kuwa; During the election process any person or member who
contravenes this code or provides false particulars or qualification, may be
penalized to a fine not exceeding five hundred thousand shillings or be barred
to participate in the election process for 2 years or for both a fine and such
barring, provided that the General Secretary lodges a complaint to the TFF
judicial organ for disciplinary action.
Kamati imebaini kuwa baadhi
ya wagombea walifanya udanganyifu kuhusu vyeti halisi walivyowasilisha kwenye
uchaguzi wa FAM na pia baadhi ya waombaji uongozi katika uchaguzi wa klabu ya
Villa. Kwa mfano mwombaji aliyeomba kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Klabu ya
Villa cheti chake cha Elimu ya Msingi alichowasilisha kwenye Kamati ya Uchaguzi
kina utata. Vyote hivyo viko katika hatua za uhakiki kwenye mamlaka husika,
uhakiki utakapokamilika Kamati itachukua hatua kwa mujibu wa Kanuni tajwa hapo
juu.
Kamati imebaini na
kujiridhisha kuwa Ndg. Michael Wambura alitoa taarifa zinazokinzana kwenye
Kamati ya Uchaguzi kuhusu umri wake. Katika Uchaguzi wa Klabu ya Simba mwaka
2010, aliwasilisha taarifa kwamba amezaliwa mwaka 1967 lakini katika uchaguzi wa
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara aliwasilisha taarifa kwamba alizaliwa
mwaka 1965. Taarifa za umri zinazokinzana za mwombaji uongozi zinashiria mashaka
ya umakini na uadilifu wa mgombea hasa ikizingatiwa kuwa nafasi ya uongozi ya
mwenyekiti kwa vyama wanachama wa TFF na Rais wa TFF zina ukomo wa
wa umri. Kamati itachukua hatua zilizoainishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi tajwa
hapo juu.
5. KAULI ZENYE LENGO LA KUVURUGA
CHAGUZI ZA WANACHAMA WA TFF.
Katika siku za
karibuni Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeshuhudia kauli amabazo si za kiwanamichezo zenye
lengo la kuleta vurugu katika michakato ya Uchaguzi. Kwa mfano kauli za
kuwahamasisha wadau wa soka kwenda mahakamani kwa masuala ya michezo, hususan,
kupinga michakato ya uchaguzi ni uvunjaji wa Kanuni za Uchaguzi na Katiba ya TFF
na FIFA. Kamati inawataka wadau wote wa soka kuheshimu na kuzingatia Kanuni na
taratibu za uchaguzi na Katiba ya TFF, vinginevyo Kamati haitasita kuchukua
hatua stahiki kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi.
Deogratias J.
Lyatto
MWENYEKITI
KAMATI YA UCHAGUZI
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU
TANZANIA