Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI mstaafu wa Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja ametuma salamu za pongezi kwa timu ya
Simba kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu ya Es Setif ya Algeria kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salam. Mgeja alituma salamu hizo jana alipozungumza na
mwandishi wa habari hizi kuhusu Simba kushinda mchezo huo wa Kombe la
Shirikisho uliopigwa juzi. Alisema ushindi huo ni heshima kwa Simba lakini pia
ni sifa kwa Taifa kutangazwa kimataifa kuwa Tanzania ina uwezo mkubwa kwenye
mchezo wa mpira wa miguu ambao una mashabiki wengi duniani. Mgeja alisema
mchezo huo uliofanyika juzi ulikuwa mgumu kwa Simba ikizingatiwa kuwa, Es Setif
ni timu kubwa na maarufu barani Afrika. Alisema ushindi wa Simba ulitokana na
uongozi thabiti wa timu hiyo kupitia kwa Mwenyekiti wake, Ismail Rage na
wasaidizi wake kwa kufanya maandalizi yaliyowezesha kupatikana kwake.
Akilielezea benchi la ufundi la timu hiyo, Mgeja alisema lilifanya kazi nzito
ya kuwaandaa wachezaji na kuzingatia mafunzo hayo kwa kumaliza dakika 90 za
mchezo wakiwa na nguvu kama waliyoanza nayo.
Alisema kipindi cha kwa nza cha mchezo huo, Simba ingejitahidi kufanya
mashambulizi ya uhakika ingeibuka na ushindi mnono wa zaidi ya mabao matano,
lakini si haba, ushindi uliopatikana unastahili kupongezwa na kila mpenda
maendeleo na mzalenzo wa nchi yake. Kutokana na ushindi huo, Mgeja alisema
kilichobakia ni kuiombea timu hiyo ifanye vizuri zaidi katika mechi ijayo ya
marudiano ambayo itaisogeza Simba katika nafasi ya juu kimichezo.