Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego akisisitiza
jambo kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki makao makuu ya Baraza hilo ambapo mada ya wiki
hii ilihusu Sanaa ya Unenguaji na Maleba katika Muziki. Kushoto kwake ni
Mwenyekiti wa CHAMUDATA, Juma Ubao na Mtendaji wa Binti Leo, Betty Kazimbaya.
Mwenyekiti wa CHAMUDATA, Bw. Ubao akieleza athari za kuwepo
kwa unenguaji usiyozingatia maadili kwenye muziki wa dansi wakati akiwasilisha
mada kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii.
Mtendaji kutoka asasi ya Sanaa za Majukwaani ya
Binti Leo Bi. Betty Kazimbaya akiongea na Wadau wa Sanaa kuhusu Umuhimu wa
Maleba Kwa Wasanii wakati akiwasilisha mada kwenye Jukwaa la Sanaa.Kulia ni
Mratibu wa Jukwaa hilo ,
Godfrey Lebejo.
Wadau wa Jukwaa la Sanaa wakifuatilia mjadala.
Na Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Sanaa la Taifa (BASATA) limeeleza kukerwa
na hali ya uvunjifu wa maadili katika sanaa hususan unenguaji na kutaka hali
hiyo sasa ifike mwisho.
Akizungumza katika Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki
makao makuu ya BASATA, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo , Bw. Ghonche Materego alisema kuwa, ni
lazima kuwe na mabadiliko dhidi ya uvunjifu maadili kwenye sekta ya Sanaa
vinginevyo hatua zitaanza kuchukuliwa.
“Haya si mambo yanayofurahisha, ni lazima jamii ioneshe
ushirikiano kwa kupambana na udhalilishaji wa aina hii, kuna mambo yasiyopaswa
kufanyika hadharani na yanabaki kuwa ya ndani tu kwenye night club na Casino na
si vinginevyo” alisistiza Materego.
Aliongeza kuwa, haivumiliki kwa maonesho hayo ya sehemu
maalum za ndani kuanza kufanywa hadharani kwani ni kinyume cha sheria na
taratibu za nchi na ni udhalilishaji wa sekta ya Sanaa hivyo aliwataka Wasanii
kujipanga kupiga vita hali hii.
“Mabadiliko lazima yafanywe. Vyama, mashirikisho na mitandao
ya Wasanii vianze mara moja kuangalia maadili kwenye maeneo yao . Hatua madhubuti zichukuliwe dhidi ya
watakaoendelea kuvunja maadili kwenye Sanaa” alizidi kusisitiza Materego.
Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania
(CHAMUDATA) Juma Ubao alisema kuwa, kinachofanyika sasa kwenye unenguaji si
muziki wa dansi bali ni aina fulani ya
matukio ambayo ni maalum kwa ajili ya night club na kasino.
“Unenguaji wa uchi usihusishwe hata kidodo na muziki wa
dansi. Haya yanayofanyika sasa ni kuuchafua muziki huu. Ni lazima tuelewe haya
si ya kuvumilia kwenye muziki wetu” alisisitiza Ubao.
Alizidi kueleza kuwa, huko nyuma wanenguaji walivaa kwa
heshima na kufanya maonesho yaliyovutia watu wa rika zote lakini kwa sasa hali
ni tofauti kutokana na kuwepo kwa vikundi vinavyovaa uchi na kuanza kunengua
hadharani.
Kwa upande wake, Mtendaji kutoka asasi ya Binti Leo
inayojishughulisha na Sanaa za majukwani Bi. Betty Kazimbaya alisema kuwa,
kinachofanyika sasa ni kudhalilisha Sanaa na ukiukwaji wa maadili kupitia
maleba (mavazi ya Wasanii) hivyo kutaka hatua zichukuliwe.
“Kazi kubwa ya maleba (mavazi ya wasanii) ni kusitiri mwili,
inakuaje kuwe na vikundi havitumii mavazi haya kwa kazi hiyo? Alihoji Kazimbaya.