John Bocco |
AZAM FC jioni hii imezima ndoto za Simba SC kutwaa mapema
ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuichapa Toto African ya
Mwanza mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi, Dar es Salaam
Azam imetimiza pointi 56 na ikishinda mechi yake ya mwisho
dhidi ya Kagera Sugar itatimiza pointi 59, sawa na za Simba iliyobakisha mechi
moja tu na Yanga Mei 5.
Iwapo Simba itafungwa na Yanga na Azam ikaifunga Kagera, ina
maana kwa mara ya pili mfululizo msimu huu, bingwa wa Ligi Kuu ataamuliwa kwa
wastani wa mabao.
Katika mchezo wa leo, Azam FC walianza kulisakama lango la
Toto huku mshambuliaji wa timu hiyo John Bocco akikosa bao baada ya kupiga
shuti lililotoka nje.
Toto African walijibu mashambulizi hayo kwa kulisakama lango la Azam lakini, Enyinna
Barlinton alikosa bao.
Azam walianza kuhesabu bao la kwanza katika dakika ya 10
kupitia kwa Kipre Tcheche huku
Tcheche akifunga bao la pili katika dakika ya 19.
Azam walizidi kuliandama lango la Toto na katika dakika ya
34, Bocco aliipatia timu yake bao la tatu baada ya kupokea pasi ya Tcheche.
Toto walifanikiwa kupata bao la kufutia machozi katika
dakika ya 85 kupitia kwa Enyiama Darlington.
Azam FC: Mwadin Ali, Erasto Nyoni, Waziri Omary, Luckson
Kakoloki, Agrey Morris, Ibrahim Mwaipopo, Mrisho Ngasa, Kipre Tcheche, Bolou
Kipre, John Bocco, Salum Salum.
Toto Africa: Mustafa Mabrouk, Idd Mobby, Eric Muliro, Peter
Mutabuzi, Ladislaus Mbogo, Laban Kambole, Emanuel Swita, Mohamed Soud, Enyiama Darlington,
Kamana Salumu, Mussa Said.