BIBI CHEKA: AJUZA MWENYE DAMU YA HIPHOP ANAYECHUKIA TAARAB


 PAMOJA na umri mkubwa alionao ameonyesha kipaji alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu; huyo si mwingine bali ni msanii wa hip hop, Cheka Hijja, maarufu kama Bibi Cheka.
Kwa mashabiki wa bongo fleva na hip hop wengi wanamfahamu msanii huyu kwani licha ya kuwa na muda mfupi tu tangu ajitose kwenye gemu hilo ameweza kujipatia umaarufu mkubwa.
Kwa siku chache tu tangu ajitose katika tasnia hiyo akifanya kazi katika  kundi la Mkubwa na Wanawe chini ya Said Fella, Bibi Cheka amepata kuwashika mashabiki wa bongo fleva kupitia singo yake ya kwanza iitwayo ‘Ni Wewe’ aliyomshirikisha Mh. Temba.
Anasema kujitosa kwake katika muziki huo si kwa kubahatisha kwani  uko kwenye damu yake hivyo kwa muda mrefu alikuwa akiwaandikia nyimbo wasanii wa muziki huo wakubwa kwa wadogo hali ambayo imemsaidia kufanikiwa kwa kazi yake ya kwanza tu.
“Hata kujiunga kwangu Mkubwa na Wanawe kumetokana na kazi hii ya uandikaji wa mashairi...kuna siku kulikuwa na ufunguzi wa ukumbi fulani huko Bunju ninakoishi ambapo Mh. Temba na wasanii wengine walialikwa kutumbuiza na hapo ilikuwa mwanzo wangu  kujitosa katika fani,” alisema.
Bibi Cheka anasema katika tukio hilo mmoja wa vijana ambao amekuwa akiwaandikia alipanda jukwaani na kuimba vema hivyo kumvutia  Mh. Temba na kumtaka kwenda kujiendeleza zaidi lakini  alimweleza kuwa yeye si kitu ila kuna Bibi anaitwa Cheka ndiye kiboko yao.
 Akizungumzia aina ya muziki anaoimba msanii huyu ni ule wa hip hop na kusema kuwa anauhusudu zaidi ya mitindo yote, huku akieleza kutoupenda muziki wa taarab.
“Mimi ninapenda sana muziki wa hip hop na ninao uwezo wa kuchana ‘kurap’ ile mbaya hilo litadhihirika katika kazi zangu zitakazofuata hivi karibuni,” aliongeza.
Hata hivyo Bibi Cheka anaeleza kutopenda kupigana vijembe katika muziki na kusema kuwa anafanya muziki kwa hamu tu na anayetaka kumfanyia hivyo amfuate nyumbani kwake Bunju.
Kuhusiana na mavazi anayovaa Bibi huyo ambayo yameonekana kuwa ya ujana zaidi tofauti na umri wake, Bibi Cheka anasema anavaa hivyo kulingana na mazingira.
“Mimi ni msanii wa hip hop siwezi kupanda jukwaani na Dera au baibui...lazima nivae suruali, raba na hata tisheti lakini nikishuka ni lazima nivae mavazi ya kujisitiri si unajua tena umri wenyewe umeshakwenda?” anasema.
Bibi Cheka anasema anavutiwa zaidi na wasanii wengi wa Ulaya lakini kwa hapa nchini amekuwa akiguswa na wasanii wanaoimba muziki wa hip hop na hasa kwa upande wa kinadada lakini kwa sasa wamekaa kando na muziki huo wakiwemo, Zay B, Sister P, Raha P na Dataz.



Historia yake 
Bibi Cheka anasema alizaliwa jijini Dar es Salaam na kukulia Ilala kabla ya kuhamia visiwani Zanzibar alipofikisha miaka 10 ambako huko alijifunza zaidi elimu ya dini ya Kiislamu.
Baadaye alirudi Tanzania Bara na kwenda kuishi kwa baba yake mzazi mjini  Morogoro kabla ya kuolewa na mume wake wa kwanza Iddi Athuman ambaye alizaa naye watoto wanne.
“Huyo mume wangu wa kwanza alikuwa baharia na tulikuwa tukiishi naye Dar es Salaam, tulipoachana nilirudi Morogoro na baada ya miaka kadhaa niliolewa tena na mchezaji wa zamani wa Simba aitwaye Juma Makwazi,” anasema.
Pamoja na muziki bibi Cheka alikuwa mpenzi sana wa mpira wa miguu ambao  aliwahi kuucheza huku akimudu zaidi kucheza namba tano.

Post a Comment

Previous Post Next Post