SIKU chache baada ya uongozi wa klabu ya
Yanga kuanza kumeguka, mwenyekiti wa klabu hiyo Lloyd Nchunga
ameitisha kikao cha dharura.
Hivi karibuni
wajumbe wawili wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo Sarah Ramadhan na Seif Ahmed
pamoja na mjumbe wa usajili Abdallah Binkleb walitangaza kujiuzuru nyadhifa zao
kwa madai ya kutoridhishwa na utendaji wa viongozi wa juu.
Habari za
uhakikika zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana zinaeleza kuwa kikao hicho
kitakachohusisha viongozi wa kamati ya utendaji kinatarajiwa
kufanyika leo jijini Dar es Salaam.
Mmoja ya viongozi
wa Yanga aliliambia gazeti hili kwamba Nchunga amelazimika kuitisha kikao hicho
cha dharura ili kujadili mustakabali mzima wa hali ya sintofahamu inayoendelea
ndani ya klabu hiyo.
Kiongozi huyo
alisema pamoja na hali hiyo, kikao hicho pia kitajadili mwenendo mzi,ma wa timu
hiyo ambayo tayari imeshapoteza ndoto za kutetea ubingwa wake baada ya kufanya
vibaya katika michezo yake kadhaa.
“Ni kweli Mwenyekiti wetu ameitisha kikao
cha dharura cha kamati ya utendaji hiyo kesho (leo) kubwa zaidi ni hali tete
inayoendelea ndani ya klabu yetu,”Alisema.
Mwandishi wa
habari hizi alipomtafuta Nchunga kwa simu yake ya kiganjani simu
yake iliita bila ya kupokelewa.
Hivi karibuni
baadhi ya wanachama wakiongozwa na mwenyekiti wa matawi ya Yanga Mohammed Msumi
waliutaka uongozi wote wa Yanga ujiuzulu baada ya kushindwa kuiletea mafanikio
timu hiyo katika msimu huu kama walivyoahidi wakati wakiomba kura.
Hata hivyo, baadhi
ya viongozi wa Yanga waliwataka Wanayanga kutulia kwanza na kuwapa
nafasi viongozi kufanya tathmini kwanza, huku Nchunga ambaye alikuwa nje ya nchi
kikazi alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa
hatojiuzulu.
Tangu kuingia
madarakani kwa Nchunga ambaye chini ya uongozi wake waliweza kutwaa mataji
matatu, mbali na hali iliyotokea hivi karibuni, kulikuwepo na msigano baina yake
na Makamu wake Mwenyekiti Davis Mosha ambaye aliamua kujiuzulu nafasi yake
hiyo.
|