TIMU ya taifa ya wanawake ya soka Tanzania , ‘Twiga Stars’ imevunja kambi yao rasmi jana hadi
Aprili 22 mwaka huu watakapokutana tena.
Kambi hiyo iliyokuwa Kambi
ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Ruvu, ilianza Machi 25, ikiwa ni maandalizi kwa
ajili ya mechi ya mchujo kuwania kufuzu Fainali za
Wanawake Afrika (AWC), zitakazofanyika Equatorial Guinea , Novemba mwaka
huu.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya
simu kutoka mkoani Pwani, Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Charles Boniface Mkwasa,
alisema kambi hiyo ilikuwa ni ya muda ili kuona uwezo wa nyota wapya aliowaita
katika kikosi hicho kwa mara ya kwanza.
“Tumevunja kambi leo mpaka Aprili 22 ndipo
tutaendelea na kambi tena, kwa ajili ya maandalizi ya michuano hiyo na kambi
hii ya muda tulikuwa tunawapa mazoezi kidogo vijana na tumeona uwezo wao kwa
kuwa ni wapya,” alisema Mkwasa.
Mkwasa alisema, katika ufundishaji wa timu hiyo,
tatizo kubwa linalomkabili ni wachezaji wanaporejea makwao, akiwaita tena kambini,
humpa wakati mgumu wa kuanza upya kile ambacho alikifundisha toka awali.
Twiga Stars katika
kibarua hicho cha kufuzu, itavaana na Ethiopia ugenini Addis Ababa Mei 26
mwaka huu, kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye jijini Dar es Salaam.