MBUNGE wa Ziwani, Ahmed Juma
Ngwali (CUF), amelishukia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuwa limejikita
kuendeleza migogoro, majungu, fitina na ubinafsi.
Ngwali, alieleza hayo bungeni
mjini hapa jana, alipokuwa akiuliza swali la nyongeza na kuongeza kuwa,
shirikisho hilo linasumbuliwa na ugonjwa wa woga, kukosa dira, muono na
utamaduni wa kifikra, katika kuendeleza soko nchini.
Kutokana na hali hiyo, alihoji
serikali ina mkakati gani wa kuendeleza soka nchini?.”
Aidha, alitaka jina la
shirikisho hilo libadilishwe, kwa madai kuwa, linahusu Tanzania Bara pekee na
liitwe Tanzania Mainland Football Federation (TMFF).
“Kwa mujibu wa Katiba, Ibara
ya kwanza na ya pili, Zanzibar ni sehemu ya Muungano na kwa kuwa, Katiba
ya TFF inatambua mikoa 21 ya Tanzania Bara na haitambui mitano ya Zanzibar. Je,
serikali haioni haja kulibadilisha jina na kuliita TMFF?” alihoji mbunge huyo.
Naibu Spika, Job Ndugai, kabla
ya kumruhusu Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella
Mukangara, kujibu swali hilo, alihoji kama ni kweli mkakati wa chombo hicho ni
kuendeleza migogoro na fitina.
Akijibu swali hilo, Naibu
Waziri huyo alisema, hakuna haja ya kulitambulisha shirikisho kuwa ni la Bara
pekee, kwa kuwa TFF inashirikiana na ZFA na kuwa hakuna mtafaruku.
“Dhana ya kutaka kuleta
mgawanyiko si sahihi,” alisema.
Kuhusu madai dhidi ya TFF, Dk.
Mukangara alisema, kazi yake kubwa ni kutatua migogoro na kuongeza kuwa
kumekuwapo migogoro katika vyama vya mipira na jukumu la shirikisho hilo ni kuitatua.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Kapteni mstaafu,
George Mkuchika, alisema kampuni nyingi zinatumia jina la Tanzania kwa sababu
kuacha kutumia jina la Tanganyika.
“ Mtuelewe, kutumia jina hili ni kwa ridhaa kati ya
ZFA na TFF na hakuna mgogoro wowote juu ya matumizi ya jina hili. Yako maelewano ya kutosha
baina ya TFF na ZFA,” alisema.
Aliongeza kuwa, hitilafu ndogo
ndogo zilizokuwepo, yalifanyika makubaliano na serikali ikafanya jitihada ya kuwakutanishwa
na kuunda kamati ya pamoja ya kuzimaliza.
Akielezea ushirikiano uliopo,
alisema, vyama hivyo viliwahi kupeleka ujumbe FIFA, kwenda kudai haki ya ZFA kuwa
mwanachama wa shirikisho hilo.
Aidha alisema misaada
inayotolewa kwa TFF kutoka FIFA, sehemu hugawiwa kwa ZFA, kama ambavyo
ilifanyika kwa fedha za kukarabati uwanja wa michezo wa Gombani, Pemba.
“Msimamo wa TFF ni
kuendelea kuungana na wenzetu wa Zanzibar, kudai uanachama wa FIFA kwa Zanzibar,
ili misaada iongezeke na nchi yetu inufaike,” alisema Mkuchika aliyewahi kuwa waziri
mwenye dhamana na michezo.