SIKU moja baada ya
kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutupilia mbali rufaa ya timu
ya Yanga kupinga kupokwa pointi tatu na mabao matatu, uongozi wa klabu hiyo
umesema bado unatafakari cha kufanya.
Kamati ya nidhamu
chini Mwenyekiti wake kamishna mstaafu wa Polisi Alfred Tibaigana iliyokutana juzi
ilitupilia mbali rufani hiyo ya Yanga iliyowasilishwa na Yanga ikilalamikia
kamati ya kamati ya Ligi kuipoka pointi
hizo na mabao matatu baada ya kumchezesha beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye
alikuwa akitumikia adhabu ya kukosa mechi tatu.
Ofisa habari wa
Yanga Louis Sendeu alisema jana kwamba wamezipata taarifa za rufaa yao
kutupiliwa mbali lakini kwa sasa wanaendelea na mambo mengine kwanza ambayo
yana manufaa na klabu hiyo huku wakiliweka kiporo suala hilo.
Alisema kwa sasa
viongozi wengi wa klabu hiyo wapo nje ya jiji la Dar es Salaam kwa majukumu
tofauti lakini bado kuna nafasi ya kukata rufaa kwa kamati ya Rufaa kama
itabidi kuwa hivyo kwa kuwa muda bado upo.
“Tumepata taarifa
za rufaa yetu kushindwa, hivyo ni mapema mno kutoa uamuzi tutkaochukua baada ya
hatua hiyo, kwa sasa tunaendelea kuchapa kazi kwanza,”alisema Sendeu.
Aprili 2 mwaka huu
Kamati ya Ligi ya TFF iliipa Coastal Union ushindi wa pointi tatu na mabao matatu
baada ya Yanga kumchezesha Cannavaro kwenye mechi ya Ligi Kuu bara kati ya timu hizo
iliyofanyika Machi 31 mwaka huu wakati akiwa na adhabu ya kukosa mechi tatu.
Kwa mujibu wa Ofisa
habari wa TFF, Boniface Wambura Yanga
katika rufani hiyo iliwasilisha sababu nane za kupinga kupokwa pointi
hizo, kubwa zikiwa Cannavaro hakustahili
kutumikia adhabu ya kukosa mechi tatu, si aliyempiga refa Israel Nkongo, ripoti
za refa na kamishna wa mechi yao dhidi ya Azam zilionesha dalili ya njama
(conspiracy) kwani zilifanana.
“Pia Cannavaro
alikuwa miongoni mwa wachezaji ambao adhabu zao zilisimamishwa na Tibaigana,
hivyo katika uamuzi wake, Kamati imesema
adhabu ya Cannavaro ya kukosa mechi tatu kwa mujibu wa Kanuni ya 25(c) ya Ligi
Kuu ya Vodacom ilitolewa na refa na si Kamati ya Ligi kama ambavyo
inalalamikiwa na Yanga, na kanuni hiyo haikatiwi rufani”, alisema Wambura.
Wambura aliongeza
kuwa barua ambayo TFF iliiandikia Yanga kuhusu adhabu ya mchezaji huyo ilikuwa
wazi kwani ilikariri kanuni ya 25(c), hivyo kitendo cha kumtumia mchezaji huyo
ulikuwa ni uzembe wa kutoheshimu kanuni na kama haikufahamu vizuri kanuni hiyo
ilikuwa na fursa ya kuiandikia TFF kwa mujibu wa Kanuni ya 25(f) ili kupata
ufafanuzi kabla ya kuamua kumtumia mchezaji huyo.
“Vilevile adhabu
zilizokuwa zimesimamishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ni zile ambazo
zilikuwa zimetolewa na Kamati ya Ligi, na si zile zilizotolewa uwanjani na refa
na kuhusu madai ya conspiracy kwa ripoti za kamishna wa mchezo huo na refa,
Kamati imebaini kuwa hazifanani, na suala lililokuwa likibishaniwa (contentious
issue) lilikuwa ni kunyang’anywa pointi tatu,”aliongeza Wambura.
Aidha, wambura
alisema kuwa Kamati ilikariri Ibara ya 50 ya Kanuni za Nidhamu za Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kuwa mchezaji anayembughudhi refa kwa njia
yoyote ile anastahili kufungiwa kwa angalau mechi sita.
mwisho