MSICHANA
mmoja aliyetambulika kwa jina la Mariam Elias, mkazi wa Misugusugu wilayani
Kibaha, mkoani hapa, amenusurika kupoteza maisha yake baada ya kunywa sumu ya
panya, kutokana na kifo cha msanii mahiri wa filamu hapa nchini, Stephen
Kanumba.
Akizungumza
na Tanzania Daima mjini Kibaha jana,
Ofisa Habari wa Shirika la Elimu Kibaha, Rose Mtei, alisema kwamba, msichana
huyo alifikishwa katika hospitali Teule ya Tumbi jana usiku, majira ya saa 5:30,
akiwa na hali mbaya kutokana na sumu aliyokunywa.
Mtei
alisema kwamba, msichana huyo wakati alipofikishwa hospitalini hapo, hali yake
ilikuwa ni mbaya, lakini madaktari waliyokuwa zamu, waliweza kujitahidi kwa
hali na mali
kumuhudumia kwa lengo la kuokoa maisha yake.
“Ni
kweli katika hospitali yetu ya Tumbi, usiku wa tarehe 10 majira ya saa 5:30, tuliweza
kumpokea msichana huyo ambaye alikuwa amekunywa sumu ya panya na alipoulizwa,
alisema ni kutokana na kifo cha nguli wa tasnia ya filamu hapa nchini, Stephen
kanumba,” alifafanua Mtei.
Aidha,
Mtei alisema kwamba, inasemekana msichana huyo alikuwa akimpenda sana marehemu Kanumba
kutokana na umahiri wake katika kuigiza filamu mbalimbali hapa nchini na nje ya
nchi.
Ofisa
huyo aliongeza kuwa, kwa sasa msichana huyo baada ya kupatiwa matibabu na
madaktari, anaendelea vizuri na kwamba, bado yupo katika uangalizi kwa ajili ya
kumfanyia uchunguzi zaidi.
Kanumba
alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita nyumbani kwake Sinza Vatican kutokana na ugomvi wa kimapenzi, kifo
kilichowagusa maelfu ya mashabiki na wadau wa filamu wa rika mbalimbali.