MUIGIZAJI wa filamu hapa nchini, Nusura
Semtawa ‘Vick’, amejigamba kuwa, picha yake mpya inayokwenda kwa jina la
‘Limbwata’ itakuwa gumzo mitaani kutokana na nyota wake kufanya mambo
makubwa.
Nusura ambaye kwa sasa anaishi
nchini Uingereza,
alitanabaisha kuwa filamu yake hiyo ni ya pili, huku akibainisha filamu yake ya
kwanza, inayokwenda kwa jina la ‘Damu ya Mjomba’ hadi leo ikiwa ni zaidi ya
miaka miwili, bado msambazaji hajaitoa.
Aliongeza kuwa ustadi katika
kuandaa filamu hiyo ni moja ya msukumo mkubwa unaomfanya aamini kwamba
‘Limbwata’ itakuwa kivutio kwa mashabiki wa ndani na nje ya
nchi.
“Filamu hii ni stori nzuri na
inasisimua sana, kwani inazungumzia jinsi baadhi ya wanaume wanavyozitelekeza
ndoa na familia zao, kwa kuhamia kwa hawara baada ya kulishwa dawa za kimapenzi
‘Limbwata’,” alijinasibu Nusura.
Aidha, alisema anaamini asilimia
100 ‘Limbwata’ italeta mapinduzi makubwa kwa waigizaji katika kuandaa filamu na
kuzipa majina ya hapa nyumbani, ukilinganisha na hivi sasa ambako nyingi
zimekuwa zikiitwa kwa majina ya kigeni.
Nusura, aliwataja nyota
walioshiriki katika filamu hiyo kuwa ni pamoja na Nurudin Mohammed ‘Chekibudi’,
Jerry Mshana ‘Jerry’, Snura, Salome na wengineo.