Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga wakati akiomba kura
BAADA ya badhi ya wanachama wa klabu ya
Yanga kuutaka uongozi wa klabu ya Yanga kujiuzulu kutfuatia kufanya vibaya kwa
timu hiyo kwenye ligi kuu soka Tanzania bara,uongozi wa umesema bado una
tathmini tatizo ni nini.
Hatua hiyo inafuati jana
timu hiyo kupokea kipigo cha bao 1-0 toka kwa Kagera Sugar hivyo kufanya timu
hiyo kuweka rehani ubingwa wake iliokuwa ikiutetetea.
Kutokana na udhaifu
iliyouonyesha timu hiyo, Mwenyekiti wa kamati ya Matawi ya Yanga, Mohammed Msumi
aliutaka uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti wake Lloyd Nchunga kujiuzulu
kutokana na kushindwa kuiletea mafanikio timu hiyo.
Akizungumza katika kituo
kipindi cha michezo cha Redio One, Msumi alisema kuwa kuna haja ya viongozi hao
kujiweka kando na timu hiyo baada ya kushindwa kutimiza ahadi zao walizoahidi
pindi walipokuwa wanaomba kura toka kwa wanachama.
“Kwa kweli tumesikitishwa
na mwenendo mbaya wa timu wetu kwenye ligi kuu bara, hivyo uongozi hauna budi
kuachia ngazi kwa sababu hakuna walichokifanya,”alisema Msumi.
Akizungumzia mtazamo huo wa
Msumi, Mjumbe wa kamati ya Utendaji ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa kamati ya
Mashindano ya Yanga Ali Mayai Tembele aliiambia mamapipiro Blog kwamba ni mapema mno kuamua
kujiuzulu ama kutojiuzulu.
Alisema wanaheshimu maoni
ya Msumi kama mwanachama wa Yanga lakini kabla ya uamuzi wowote kamati ya
Utendaji haina budi kukutana na kutathmini kwa kiasi gani tumefanikiwa au
kutofanikiwa ndipo tutawaeleza wanachama.
“Mzee wetu Msumi ana haki ya kusema kile
anachokifikiria kutokana na hali halisi ilivyo lakini ni vigumu kwa mtu mmoja
mmoja kufanya maamuzi ni lazima tukutane kama kamati na kujadili mambo
yanavyokwenda,”Alisema Mayai.
Mchezaji huyo wa zamani wa
Yanga na timu ya Taifa aliongeza kuwa hata uongozi pia umesikitishwa na mwenendo
wa timu hiyo , hivyo hawanabudi kukaa chini na kuangalia tatizo ni
nini.
Yanga ambayo inashika
nafasi ya tatu kwenye ligi hiyo ikiwa na pointi 43 nyuma ya Azam yenye pointi 50
na Simba inayoongoza ligi hiyo iliwa na pointi 56, imeshafifisha ndoto zake za
kuwania ubingwa huo.