HOMA ya
mpambano wa ligi kuu bara baina ya watani wa jadi nchini Simba na Yanga imeanza
kupanda ambapo leo timu hizo zimeingia kambi kujiandaa na mpambano wao
utakaopigwa Mei 5 kwenye dimba la taifa.
Wakati
Yanga ikiingia kambini katika hosteli zilizopo klabuni kwao mitaa ya Jangwani
na Twiga, Simba wameelekea Visiwani Zanzibar ambapo mara nyingi huenda
kujiandaa na michezo muhimu ikiwemo dhidi ya Yanga.
Habari ambazo mamapipiro blog imezipata jijini Dar es Salaam, zinaeleza kwamba Simba imekwenda Zanzibar kwa ajili ya
kunoa makali na itarejea siku moja kabla ya mechi ama siku ya mechi.
“Vijana
wameondoka mchana huu kwenda Zanzibar kwa
ajili ya kwenda kusaka makali ya kuwaua Yanga, hivyo nadhani watakaa kule kwa
siku tatu au nne na kurejea jijini Dar
es Salaam ,”Alisema kiongozi mmoja wa Simba.
Kwa upande
wa Yanga ambayo kwa siku za hivi karibuni imeonekana kutetereka na hatimaye
kuutema ubingwa wake, kama mambo yakienda
vizuri nayo huenda ikahamisha kambi yake.
kiongozi
mmoja wa Yanga ambaye hakupenda kutajwa jina lake alisema
jana kwamba wanaangalia uwezekano wa kuihamisha timu kutoka Jangwani hadi
mahala pengine iwe ndani au nje ya jiji la Dar es Salaam.
Mchezo
baina ya timu hizo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na historia
iliyonazo timu hizo pindi zinapokutana kwa miaka kadhaa hivi sasa ambapo katika
mzunguko wa kwanza, Yanga iliifunga Simba bao 1-0 lililopachikwa na Mzambia
Davies Mwape.
Wakati
Simba inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 59, Yanga inashika nafasi ya tatu
ikiwa na pointi 49.