MSAFARA wa timu ya Simba, ulirejea jana
asubuhi na kulakiwa kwa kishindo
baada ya kuwang’oa ES Setif ya Algeria
katika michuano ya Kombe la Shirikisho, lakini wakiwa na majonzi ya kuibiwa
fedha na simu katika hoteli waliyokuwa wakiishi.
Timu hiyo iliyokuwa imefikia kwenye
Hoteli ya Zidane; mali ya nyota wa kimataifa
wa zamani wa Ufaransa, Zinedine Zidane
mwenye asili ya Algeria, imeibiwa jumla ya dola 400 za Marekani na simu ya
mkononi.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuwasili
jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage, alisema wizi
huo ulifanyika katika hoteli hiyo siku ya Ijumaa wakiwa uwanjani kucheza na
Setif.
Alisema, walibaini kuibiwa baada ya
kurejea kwenye hoteli hiyo; wakati huo wakiwa mashujaa kwa kuwatupa nje ya
michuano wapinzani wao ES Setif,
licha ya kufungwa mabao 3-1, wakibebwa
na bao la ugenini la Emmanuel Okwi
Rage alifafanua kwamba, waliobiwa fedha
ni mchezaji Derrick Walulya na Mwinyi Kazimoto ambaokila mmoja amelizwa kiasi
cha dola 100 za Marekani huku Kocha Msaidizi, akikombwa dola 200 za Marekani.
Iwe ni wizi wa kawaida hotelini au
hasira ya kung’olewa kwenye michuano hiyo, Rage kwa upande wake ameibiwa simu
ya mkononi hadi wanaondoka katika
ardhi ya Algeria, vitu hivyo vilishindwa
kupatikana.
Nje ya mkasa huo, mamia ya mashabiki wa
timu hiyo jana ashubuhi walijotokeza kuwalaki mashujaa hao kwenye Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, baada ya kutinga
raundi ya pili ya michuano hiyo.
Licha ya kuwasili majira ya saa 12
asubuhi, tayari wapenzi na mashabiki wa timu hiyo walikuwa wamefika kuwapokea
mashujaa hao waliowang’oa ES Setif kwa
bao la ugenini baada ya kufungana jumla ya mabao 3-3.
Katika mechi ya kwanza iliyopigwa Machi
25 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini
Dar es Salaam, Simba walishinda 2-0, hivyo
kwa kufungwa 3-1 katika mechi
ya marudiano, wakabebwa na bao la ugenini.
Baada ya kuwasili, msafara wa timu hiyo
ulilakiwa kwa shangwe na nderemo zikipambwa na sauti za vuvuzela, pikipiki,
magari na ngoma kutoka kikundi cha wakereketwa wa timu hiyo maarufu kwa jina la
Kidedea.
Baada ya kuwasili, msafara ulianza
kupita barabara ya Nyerere, Kawawa na Uhuru hadi Makao Makuu ya klabu hiyo,
Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam huku mashabiki wengi wakitembea kwa
miguu wakifuatana na msafara wa magari yaliyobeba viongozi na wachezaji.
Akizungumza mara baada ya kuwasili, Kocha
Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic, alisema, siri ya mafanikio ya timu yake ni
maandalizi mazuri ambayo walifanya kuelekea mechi hiyo.
“Mchezo ulikuwa mgumu sana, hali ya hewa
ilituathiri sana, lakini wachezaji wangu niliwaandaa vizuri kisaikolojia, tukafanikiwa
kutinga hatua ya pili ya 16 bora,” alisema.
Akitoa hotuba fupi Makao Makuu ya klabu
hiyo, Mwenyekiti wa Simba, Rage, alisema katika mechi hiyo ngumu, wakitumia
uzoefu wao, walipambana dhidi
ya fitna za ndani ya nje ya dimba
zilizofanywa na wenyeji wao.
Nahodha wa Simba, Juma Kaseja, alisema
nia yao ni kuhakikisha wanasonga
kila hatua kwani hesabu zao ni kucheza
hatua ya nane bora, nusu fainali hadi fainali ya michuano hiyo.
“Tuko vitani na nia yetu ni kupambana na
hatimaye kufika makundi, nusu na hatimaye fainali, Tunahitaji sapoti ya kila
Mtanzania kutuwezesha kufanikisha hili,” alisema Kaseja.
Baada ya Simba kuitoa ES Setif ya
Algeria, sasa itapambana na Al Ahli Shendi ya Sudan, ambayo katika michezo yake
miwili imeweza kuitoa nishai Ferroviario de Maputo ya Msumbiji kwa jumla ya
mabao 3-0.
Naye mfungaji wa bao hilo pekee la Simba,
Okwi, alisema ushindi huo umetokana na juhudi na
ari ya wachezaji ambayo walikuwa nayo
wakati wote wa mechi hiyo iliyokuwa ngumu kwao.