WAZIRI wa
Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk
Mwinyihajji Makame amesema kwamba rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
Leodegar Chillah Tenga anavuruga Muungano katika michezo kwa kuitenga
Zanzibar.
Katika mahojiano maalum na bongostaz.blogspot.com
mchana huu katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort visiwani hapa, Dk Makame
amesema kwamba TFF ya Tenga imekuwa ikichukua maamuzi mengi mazito kuhusu
masuala ya soka yenye kugusa maslahi ya pande zote mbili, bila kuwashirikisha
ZFA (Chama cha Soka Zanzibar).
Dk Makame ametolea mfano muundo wa timu ya taifa,
Taifa Stars kuanzia uteuzi wa kocha na hata suala la udhamini wa timu, Zanzibar
huwa hawashirikishwi jambo ambalo amesema ni baya ni linahatrisha muungano
katika michezo nchini.
Dk Makame amesema kwa sasa anasikia timu ya
taifa inataka kubadilishwa jina kutoka Taifa Stars na kuwa Kili Stars, jina
ambalo linatokana bia ya wadhamini wapya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na
anakitika maamuzi hayo yanachukuliwa bila Zanzibar kushirikishwa.
“Siungi mkono suala la Taifa Stars kubadilishwa
jina, naomba Wizara husika zote mbili, zisimamie hilo lisijitokeze,”alisema.
Dk Makame, ambaye pia ni Mlenzi wa timu ya Ikulu
SC amesitikishwa na kitendo cha TFF kutoikumbuka ZFA katika migawo wanayopata
kutoka FIFA.
Aidha, Dk Makame alisema kwamba muundo wa TFF pia
unapaswa kurekebishwa, ili uendane na muundo wa serikali mbili katika nchi
hii.
“Kuna serikali ya Muungano na serikali ya
mapinduzi, katika serikali ya mapinduzi tuko wenyewe kwa sababu tunasimamia
mambo yetu tu huku, lakini serikali ya Muungano ipo kwa ajili ya taifa letu
zima, inahusisha watu wa pande zote mbili. Utaona Rais anatoka Bara, lakini
Makamu wake anatoka Zanzibar.
Vivyo hivyo,
katika muundo wa Baraza la Mawaziri pia, unahusisha pande zote mbili, lakini
ndani ya TFF, Zanzibar haihusishwi kabisa, hii si sawa na matokeo yake soka ya
huku inazidi kudidimia kwa sababu hatunufaiki hata migawo ya FIFA,”alisema.
“Tunampenda sana Tenga, tangu akiwa mchezaji,
Kocha na sasa kiongozi, rais wa TFF, CECAFA na anaiwakilisha vema nchi yetu kwa
kweli, ila lazima ahakikishe anatenda haki,”alisema.
Aidha, kwa upande wake Naibu Waziri wa Habari
Utamaduni Utalii na Michezo, Bi Hindi Hamad Khamis amelaani vikali pia desturi
ya TFF kuitenga ZFA.
Bi Hindi, ameiambia bongostaz.blogspot.com mchana
huu katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort visiwani hapa kwamba anasikia hivi
sasa timu ya taifa inataka kubadilishwa jina na kuwa Kili Stars wakati timu hiyo
ni ya muungano na ZFA hawajashirikishwa.
“Si haki kutoishirikisha ZFA ndani ya TFF, lazima
kuwe na ushirikiano kama tulionao kwenye serikali yetu ya Muungano.
Bi Hindi alipoulizwa kama amefanya jitihada
zozote za kukutana na Wizara inayohusika na Michezo katika serikali ya Jamhuri
ya Muungano, alisema; “Unajua hivi karibuni yamefanyika mabadiliko ya Baraza la
Mawaziri huku kwetu, ila Waziri aliyepita hakika alifanya hivyo na mimi napenda
niwaahidi wapenzi wa michezo Zanzibar na Wazanzibari kwa ujumla, kwamba
tutafuatilia,”alisema Bi Hindi.
Naye Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi jimbo la
Raha Leo (CCM), Nassor Salim Ali ‘Al Jazeera’ amelaani vikali pia kitendo cha
TFF kutoishirikisha ZFA katika masuala ya soka yenye kugusa maslahi ya pande
zote mbili.
Al Jazeera aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa ZFA
Wilaya ya Mjini Magharibi, alisema kwamba naye amesikia juu ya mpango wa timu ya
taifa kutaka kubadilishwa jina na kuwa Kili Stars, lakini anapinga.
“TFF hawawezi kubadilisha jina la timu ya taifa
inayoihusisha na Zanzibar pia, bila kuishirikisha ZFA, hii si sawa na mbaya
zaidi jina lenyewe ni la pombe kitu ambacho kipo tofauti na sisi kimaadili
yetu,”alisema.
Al Jazeera alisema Zanzibar wamekuwa wakijitahidi
kulinda Muungano katika michezo na ndiyo maana kila mwaka katika Kombe la
Mapinduzi hualika timu za Bara.
Lakini amesema anasikitika TFF au Bara kwa ujumla
wanaitenga Zanzibar. “Timu ya taifa ni yetu sote, lakini haiji kucheza huku hata
mechi za kirafiki, wakati sisi tunakuwa wenyeji wa michano mikubwa tu ya CECAFA
hapa. Tunakosaje sifa za kuandaa mechi ya timu ya taifa, japo ya
kirafiki?”alihoji Al Jazeera.
Vigogo hawa wanatoa malalamiko hayo, katika
wakati mwafaka kwani ni leo Mkutano Mkuu wa TFF umeanza katika ukumbi wa NSSF
Water Front, Dar es Salaam na unatarajiwa kufungwa kesho.
CHANZO:BONGO STAZ BLOG