Afisa
kutoka Kampuni ya uhakiki wa mahesabu ya Innovex, Edna Masalu akieleza juu ya
utaratibu wa kupiga kura kwenye tunzo za muziki Tanzania wakati akiwasilisha
mada kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki makao makuu ya BASATA.
Katikati ni Lloyd Zhungu kutoka Innovex na Mratibu wa Jukwaa hilo, Agnes
Kimwaga.
Mratibu
wa Tunzo za Muziki Tanzania kutoka BASATA, Bw. Angelo Luhala akisistiza jambo
kuhusu tunzo hizo. Pamoja na mambo mengine alitoa wito kwa watanzania kuziona
tunzo hizo kama kitu chao wanachopaswa kujivunia.
Msanii
Khamisi Ramadhan aka H Baba naye alikuwa miongoni mwa wadau wa Jukwaa la Sanaa
waliotoa maoni yao kuhusu zoezi la upigaji kura kwenye tunzo za muziki
Tanzania.
Mzee Rashid Masimbi ambaye ni moja ya wadau wanaoheshimika kwenye tasnia ya Sanaa nchini akitoa maelekezo na ufafanuzi kuhusu tuzo za muziki huku wadau wakimsikiliza kwa umakini.
Na
Mwandishi Wetu
Zoezi
la upigaji kura kwa ajili ya kuwapata washindi wa tuzo za muziki Tanzania kwa
mwaka 2012 linatarajia kufikia kikomo wiki hii huku wito ukitolewa kwa wadau wa
Sanaa kuendelea kuwachagua wasanii wao.
Akizungumza
kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii makao makuu ya Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA), Afisa kutoka Kampuni ya ukaguzi na uhakiki wa mahesabu ya Innovex
ambayo ndiyo yenye jukumu la kuratibu zoezi zima la upigaji kura Edna Masalu
alisema kuwa, mchakato wake unaendelea vema na unatazamia kufika kikomo wiki
hii.
“Zoezi
la upigaji kura lililodumu kwa zaidi ya mwezi mmoja na nusu litafikia mwisho
wiki hii Aprili 6, wadau wa muziki wanahamasishwa kuendelea kuwachagua wasanii
wenye kazi wanazoona ni bora katika kipindi hiki ili kuwawezesha kushinda”
alisema Edna.
Kuhusu
umakini kwenye zoezi la kupiga kura, Edna alisema kuwa, Kampuni ya Innovex
imebuni njia mbalimbali za upigaji kura ili kuwawezesha wadau wa Sanaa wa kada
mbalimbali kuweza kupata fursa ya kupiga kura na kuwa sehemu ya tuzo hizo zenye
umaarufu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Alizitaja
njia hizo ambazo zinatumika kupiga kura kuwa ni pamoja na ujumbe mfupi wa simu
ya mkononi kupitia namba maalum, magazeti, vipeperushi na mitandao ya kompyuta
ambapo alisisitiza kwamba, kila mtanzania ana haki ya kupiga kura moja tu kwa
kila eneo (category) inayoshindaniwa.
“Hakuna
njia yoyote ya upendeleo, kura zinapigwa na kuhesabiwa kwa uwazi kupitia
mtandao. Toka Academy imeanza hadi sasa zoezi la upigaji kura kwa watanzania
mfumo ni wa wazi na hakuna mwanya wa upendeleo”
alisisitiza.
Awali,
akiongea kuhusu tuzo hizo, Mratibu kutoka BASATA Angelo Luhala alisema kuwa,
wasanii na wadau wa Sanaa wanapaswa kuthamini tunzo hizo kama kitu chao kwani ni
kitu kilichobuniwa na watanzania kwa ajili ya kukuza muziki
nchini.
“Malengo
ya tuzo hizi ni kukuza muziki nchini na kuwapa ari wasanii wabuni kazi zenye
ubora. Ni wazi msanii anayepata fursa ya kuwa kwenye moja ya kipengele
kinachoshindaniwa ni heshima kubwa” Alisisitiza
Luhala.
Tuzo
za muziki Tanzania kwa mwaka 2012 zinatarajia kufikia kilele chake Aprili 14
mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mlimani City ambapo wasanii mbalimbali watatambuliwa
na kutuzwa.