Siku chache baada ya kutokea kifo cha msanii nguli na
mwanzilishi wa Bongo Movies Marehemu Steven Kanumba; Tasnia ya mitindo
imeelezea ni kwa jinsi gani imeshtushwa na kusikitishwa na kifo cha nguli huyo
wa filamu si tu nchini Tanzania bali Afrika kwa ujumla wake.
Marehemu Steven Kanumba alikuwa na mchango mkubwa sana katika kuendeleza si tu Sanaa ya maigizo, bali pia
Ubunifu wa mitindo kwa kuhudhuria maonyesho mbalimbali ya mitindo ya mavazi Tanzania kama
Swahili Fashion Week, Red Ribbon Fashion Gala, Lady In Red na kadhalika.
Akimzungumzia marehemu Steven Kanumba kwa niaba ya Tasnia ya
Ubunifu wa mavazi, mbunifu nguli wa mavazi Afrika Mashariki na Kati Mustafa
Hassanali alisema “Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa hizi, Kanumba
ameondoka katika kipindi ambacho taifa linauhitaji mchango wake san. Ni majonzi
mazito si tu kwa tasnia ya filamu bali pia kwa tasnia ya ubunifu wa mitindo,
kwani Kanumba alijikita katika kutangaza mavazi yaliyobuniwa na wabunifu wa
hapa nyumbani, hakuwa balozi wa filamu tu bali pia balozi wa mitindo Tanzania ”
“Kanumba ni kijana thabiti aliyekuwa akisimamia ukweli,
uwazi, uwajibikaji na kile alichokiamini kuwa ni haki. Ama kwa hakika atakumbukwa
kwa mengi na pengo lake
halitaweza kuzibika”.
Aliongeza Hassanali.
Tasnia nzima ya ubunifu wa mitindo inasikitika sana
kuondokewa na mpendwa wetu Ndugu Steven Kanumba na inatoa pole za dhati kwa
ndugu, jamaa, marafiki, wanafilamu, mashabiki wake na watanzania wote kwa
ujumla. Tulimpenda sana
ila Mwenyezi Mungu kampenda zaidi, na kazi yake siku zote haina makosa. Pumzika
kwa Amani. Amin