Na Edson Kamukara
KAMBI ya Rasmi ya Upinzani
bungeni imeeleza kushangazwa kwake na hatua ya Serikali kushindwa kuwa na
takwimu za kiasi gani cha fedha zimepatikana kama
stahiki yake ya kodi kutoka kwenye sekta ya michezo hususani uuzaji na ununuzi
wa wachezaji kwa timu za ndani na nje.
Pia, kambi hiyo iliitaka
serikali kueleza wazi ni uwekezaji gani unaofanyika kwa lengo la kupata faida
na baada ya muda gani kutokana na uwekezaji wa sh bilioni 56.4 uliofanywa na serikali
kwenye uwanja wa michezo wa Taifa.
Kauli hiyo ilitolewa jana na
msemaji wa kambi hiyo kwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,
Joseph Mbilinyi (Chadema), wakati akiwasilisha maoni ya upinzani
kwa wizara hiyo.
Alisema, ni mara nyingi
wamekuwa wakiishauri serikali kuanzisha uwekezaji mkubwa katika sekta ya
michezo kwa ujumla, lakini mapendekezo na ushauri wao vimeshindwa kuchukuliwa
kwa umakini.
Kuhusu malipo ya makocha
wazalendo, Mbilinyi maarufu kama Sugu, alisema yapo malalamiko ya muda mrefu ya
makocha hao wanaofundisha timu za ndani kulipwa ujira kiduchu mno
ikilinganishwa na wageni.
“Kambi ya upinzani inataka
serikali kutoa majibu kuhusu
hatua iliyofikiwa kuhusiana
na maandalizi ya mikataba kwa makocha wazalendo. Hii ni kwasababu katika
randama iliyotolewa na Wizara kuhusu fungu 96, ukurasa wa 27 serikali imetenga
sh milioni 400 kwa
ajili ya makocha wa kigeni,”
alihoji.
Akizungumzia viwanja vya
michezo, Mbilinyi alisema wanapendekeza vile vinavyomilikiwa na CCM virejeshwe
serikalini vitumiwe na wananchi wote bila kujali itikadi lakini pia hatua hiyo
ni baada ya chama hicho kushindwa kuviendeleza.
Alisema, hiyo imevifanya
viwanja hivyo kukosa hadhi ya kutumika kwenye mashindano ya kimataifa.
Katika sekta ya utamaduni,
kambi ya upinzani imeitaka serikali kuweka msimamo wake wazi kuhusu mashindano
ya Big Brother Africa kwani licha ya kuyapinga ikidai hayaendani na tamaduni na
mila za kitanzania, bado yanaendelea kuoneshwa na Watanzania wanashiriki.
Mbilinyi pia aligusia kazi
za wasanii ambapo licha ya kumpongeza Waziri aliyepita katika wizara hiyo, Dk.
Emmanuel Nchimbi kuwa alijitahidi, alisema kuwa pendekezo lao la kuitaka wizara
kuunda kikosi kazi kufanya kazi ya kutafiti namna ya kilinda kazi za wasanii
nchini, bado inasuasua.
Naye mbunge wa Kinondoni,
Idd Azzan (CCM), aliiunga mkono hoja ya Mbilinyi kuhusu viwanja vya CCM akisema
kuwa ni licha ya kumilikiwa na chama hicho, bado mapato yanasimamiwa na TFF,
hivyo akaitaka serikali kuviendeleza.
Mbunge wa Viti Maalum, Grace
Kihwelu (Chadema), katika hilo
aliwataka CCM wasione ugumu kwani hatua hiyo itakuza michezo nchini maana chama kimeshindwa kuvihudumia na
kuingiza mapato makubwa kwa serikali.
Kuhusu timu ya soka ya Taifa
ya wanawake, Twiga Stars, Kihwelu alidai kuwa serikali imekuwa ikionesha
upendeleo kwa timu ya wanaume, ‘Taifa Stars,’
hivyo ya wanawake kutembeza bakuli kwa wafadhili licha ya kufanya vizuri
katika mashindano ya kimataifa.
“Twiga Stars inahitaji
kuhudumia kama Taifa Stars, wachezaji hawa nao wanapaswa kuwekewa bima kama
wenzao wanaume ili wakiumia wawe na uhakika wa matibabu lakini vile vile
wanapaswa kulazwa mahali pazuri na kulishwa chakula kizuri,” alisema.