TABORA MARATHON YAWASHUKURU WADAU


Mshauri wa Ufundi wa Tabora Marathon Tullo Chambo kulia, akishiriki mbio hizo  mjini Tabora

Na Mwandishi Wetu
 
KAMATI ya mbio za Tabora Marathon imewatunukia vyeti maalumu vya shukrani wadau mbalimbali waliofanikisha kufanyika kwa mbio hizo za kwanza Machi 10 mwaka huu mjini Tabora.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Tabora Marathon , Ramadhani Makula, baada ya vikao vya tathmini, wameazimia kuwashukuru wale waliofanikisha mbio hizo, ambako tayari Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwassa, tayari kakabidhiwa cheti hicho.
“Unajua serikali ya mkoa wetu wa Tabora chini ya mama yetu Fatma Mwassa, walituunga mkono sana kufanikisha mbio hizi, maana ilikuwa ni mara ya kwanza na wadau wengi walikuwa hawajaitambua na kuikubali, hivyo kuwa wagumu kutuunga mkono,” alisema Makula.
Mratibu huyo aliongeza kuwa, baada ya RC Mwassa, zoezi la kuwapa vyeti wadau wengine waliopo jijini Dar es Salaam litafanyika.
Wadau hao ni pamoja kampuni ya Kishen Enterprises ambao ni wasambazaji wa pikipiki za Toyo, Azania Wheat Flour, NGS na mdau wa michezo, Sarah Ramadhani ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Klabu kongwe ya Yanga.
Kwa upande wake, Mshauri wa Ufundi wa Tabora Marathon , Tullo Chambo, alisema, maandalizi kwa ajili ya mbio za mwakani tayari yameanza na kuwa, kutakuwa na mabadiliko makubwa kwa lengo la kuziboresha.
Aliwataka wakazi wa Tabora na Kanda ya Magharibi kwa ujumla, kujikita katika mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mbio za mwakani ili waweze kufanya vema na kujinyakulia zawadi mbalimbali.

Post a Comment

Previous Post Next Post