KLABU ya soka ya Simba jana imepokea msaada wa jezi, raba, viatu
vya kuchezea mpira, mabegi na suti za michezo (tracksuit) – vyote vya kisasa
kabisa, kutoka kwa familia ya Al Ruwahi. Msaada huo umetolewa kwa mapenzi mema
ambayo familia hiyo inayo kwa klabu.
Ikumbukwe kwamba mahusiano baina ya familia ya Al Ruwahi (Ruwehi)
na Simba yamedumu kwa zaidi ya miaka 30 sasa. Takribani miaka 30 iliyopita,
familia hiihii ilitoa zawadi ya basi (Nissan Coaster) kwa Simba na kuifanya
klabu yetu kuwa ya kwanza nchini kumiliki basi lake yenyewe .
Msaada huo wa sasa kwa Simba una thamani ya Sh milioni 18
kwa ujumla wake na Simba sasa itavaa jezi hizo katika pambano lake la kesho
dhidi ya Azam katika michuano ya Kombe la Kagame.
Klabu ya soka ya Simba inatumia nafasi hii kuwakaribisha
wapenzi na wanachama wake kujitokeza kuisaidia klabu kwa namna yoyote ile, kama ilivyofanya familia hii ya Al Ruwahi, ili kusukuma
mbele gurudumu la maendeleo ya klabu.
Simba ni ya kila mmoja na haina mwenyewe. Umoja na
mshikamano baina ya viongozi, wadhamini, wapenzi na wanachama wake, ndiyo
utakaoifanya izidi kuwa bora hapa nchini na nje ya mipaka ya taifa letu.