KATIBU mkuu wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) Angetile Osiah ametangaza kujivua nafasi yake ya ujumbe wa
kamati ya uchaguzi ya klabu ya soka ya Yanga.
Osiah amesema kuwa analazimika kufanya hivyo kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi
za shirikisho hilo na atawasilisha barua kwa katibu mkuu wa Yanga, Mwesiga
Selestine.
Alisema kuwa licha ya
kuteuliwa muda mrefu kushika wadhifa wa ukatibu wa TFF, alishindwa kuwasilisha
barua ya kujitoa katika kamati ya uchaguzi kutokana na kuingwa na majukumu
ndani ya shirikisho hilo .
“Nimelazimika kufanya hivyo
kwani kwa sasa Yanga inahitaji kufanya uchaguzi mdogo kwa lengo la kuziba
nafasi zilizoachwa wazi na baadhi ya viongozi walioachia ngazi Yanga hivyo
inabidi nafasi yangu ijazwe ili kamati iweze kuendesha mchakato wake
kikamilifu,”alisema.
TFF kupitia kamati ya
uchahizi iliyo chini ya mwenyekiti wake Deogratius Lyato iliiagiza kamati ya
uchaguzi ya Yanga chini ya mwenyekiti wake Jaji John Mkwawa ifanye uchaguzi
wake kuziba nafasi za nane za viongozi waliojiuzulu na mjumbe mmoja aliyefariki
dunia.
Hatua hiyo inafuati hivi
karibuni kujiuzulu kwa mwenyekiti wa Yanga Lloyd Nchunga kutokana na shinikizo
la baadhi ya wanachama wakiongozwa na baraza la Wazee waliomtaka kufanya hivyo
kwa madai ya kutoiletea mafanikio klabu na hatimaye kupokwa ubingwa wao wa ligi
kuu bara ulioenda kwa Simba na wao kuishia nafasi ya tatu.
Awali makamu mwenyekiti wa
Yanga Davis Mosha alitangaza kujiengua katika uongozi miezi michache baada ya
kuchaguliwa kwa madai ya kutoelewana na Nchunga, huku mjumbe wa kamati ya
utendaji, Theonest Rutashoborwa alifariki dunia.
Kama hiyo haitoshi, wajumbe
wengine walioachia ngazi Yanga ni pamoja na Seif Ahmed, Mbaraka Igangula, Mzee
Yusuf, Ally Mayay, Charles Mgondo na Mohammed
Bhinda.