Timu ya Taifa ya wanawake ya Afrika Kusini (Banyana Banyana) inatarajia kuwasili nchini leo (Mei 18 mwaka huu) saa 12.45 jioni kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Twiga Stars itakayofanyika Jumapili (Mei 20 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Banyana Banyana ina msafara wa watu 26 ambapo 18 kati ya hao ni wachezaji na itafikia kwenye hoteli ya Sapphire Court Hotel tayari kwa mechi hiyo ya kujipima nguvu kwa Twiga Stars inayojiandaa kwa mechi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Ethiopia. Mechi dhidi ya Ethiopia itachezwa Mei 27 mwaka huu jijini Addis Ababa.
Nayo Banyana Banyana iko katika kinyang’anyiro cha kutafuta tiketi ya Fainali za AWC ambapo katika raundi hii ya pili imepangiwa Zambia na itaanzia mechi hiyo ugenini jijini Lusaka.
Kesho (Mei 19 mwaka huu) saa 6 kamili mchana, makocha wa timu zote mbili, Boniface Mkwasa wa Twiga Stars na Joseph Mkhonza wa Banyana Banyana watakuwa na mkutano na Waandishi wa Habari kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuzungumzia mechi hiyo.
Twiga Stars na Banyana Banyana zote ziko katika raundi ya mwisho ya AWC ambapo zikifanikiwa kuwatoa wapinzani wao zitakwenda kwenye fainali hizo zitakazofanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.