KESI YA LULU YAPIGWA TENA KALENDA


Na Happiness Katabazi 
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana iliahirisha tena kesi ya mauaji ya msanii nyota wa filamu nchini, Steven Kanumba, inayomkabili Elizabeth Michael ‘Lulu’ hadi Juni 4, kwa maelezo kuwa jalada la kesi hiyo limeitwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Lulu kupitia mawakili wake Kenned Fungamtama, Peter Kibatara, Fulgence Masawe na Joaquine De- Melon, Mei 15 mwaka huu,  aliwasilisha ombi Na.46/2012 chini ya hati ya dharura iliyokithiri Mahakama Kuu, akiomba iamuru Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kulishughulikia ombi lake la kutaka kesi hiyo isikilizwe katika Mahakama ya Watoto kwa sababu ana umri chini ya miaka 18.
Mei 18 mwaka huu, uongozi wa Mahakama Kuu ukampangia Jaji Dk. Fauz Twaibu kusikiliza ombi hilo, ambalo atalisikiliza Mei 28 mahakamani hapo.
Kwa mujibu wa ombi hilo, Lulu ambaye pia ni msanii wa filamu, anadai kuwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu Augustina Mmbando Mei 7 mwaka huu, alikataa kutoa uamuzi wa kutaka kesi hiyo ihamishiwe katika mahakama ya watoto na badala yake akasema mahakama hiyo haina mamlaka na kuwashauri mawakili wake kuwasilisha ombi hilo Mahakama Kuu.
Wakili Fungamtama alidai katika hati hiyo ya madai kuwa, Hakimu Mmbando alijielekeza vibaya kwa kusema kuwa mahakama ile ilikuwa haina mamlaka ya kusikiliza ombi lao, kwa hiyo wanaiomba Mahakama Kuu imwelekeze hakimu huyo asilikize ombi lao na alitolee maamuzi na kuwa endapo itabaini vinginevyo basi mahakama hiyo ya juu itoe tafsiri ya umri kuhusu ombi hilo.
Lulu alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Aprili 11, mwaka huu akitajwa kuwa mshukiwa namba moja katika kesi ya kifo cha Kanumba kilichotokea Aprili 7, mwaka huu nyumbani kwake maeneo ya Vatican, Sinza jijini Dar es Salaam.


Post a Comment

Previous Post Next Post