MWIGIZAJI mkongwe wa vichekesho nchini, Saidi Ngamba,
maarufu kwa jina la Mzee Small, amelazwa katika Hospitali ya Amana, Ilala
jijini Dar es Salaam ,
baada ya kuugua ghafla.
Mzee Small anayesumbuliwa na maradhi ya shinikizo la damu
kiasi cha kushindwa kuongea; aliugua ghafla juzi jioni muda mfupi baada ya
kutoka Mwanza alikokwenda kwenye shughuli za kisanii.
Mwigizaji mwenzake Chausiku
Salum Maele ‘Bi Chau,’ alisema kabla ya kuugua, Mzee Small alikuwa mwenye afya
njema, hadi walipoachana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA) walikirejea kutoka Mwanza.
Kwa mujibu wa Bi. Chau, walikwenda Mwanza Ijumaa iliyopita
kusherehesha shughuli ya walemavu wa ngozi ‘Albino,’ iliyoandaliwa na madaktari
wa Hospitali ya Bugando, jijini humo.
“Tuliondoka Dar es Salaam na ndege ya jioni Ijumaa tukalala
Mwanza, Jumamosi tukafanya kazi iliyotupeleka. Jumapili jioni tuliondoka Mwanza
kuja Dar, sasa kabla sijafika nyumbani kwangu Magomeni nikapokea simu kutoka
kwa binti yake Small, akanipa taarifa za ugonjwa, nilishtuka,” aliongeza Bi
Chau swahiba wa nguli huyo wa vichekesho.
Tanzania Daima ikampigia mke wa Mzee Small, ambapo alisema
bado hali ya mumewe haijatengemaa hivyo kuomba dua za Watanzania.
“Ana tatizo la presha na huwa anajikuna na kuvimba, lakini
safari hii amevimba shavu moja na kadiri muda unavyokwenda hali yake inazidi
kuwa mbaya,” alisema mke huyo akiwa nyumbani kwake Tabata Kimanga kabla ya
kumpeleka hospitali.
Katika maelezo ya mke huyo wa Mzee Small, alisema juzi usiku
walimpeleka mumewe Hospitali ya KLM iliyoko Tabata, ambapo alipewa dawa ya
kupunguza shinikizo la damu kisha kuruhusiwa kurudi nyumbani na kwamba hali ya
msanii huyo iliendelea kuwa mbaya hadi alipokimbizwa Hospitalli ya Amana jana
mchana.
CHANZO:GAZETI LA TANZANIA DAIMA
Bosi wangu mbona picha hauweki niaje?
ReplyDelete