RIADHA TANZANIA WAPATA VIONGOZI WAPYA


WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), wamempa kura za kishindo Antony Mtaka  kuwa Rais wa Shirikisho hilo akimbwaga Kanali mstaafu, Juma Ikangaa.
Katika nafasi hiyo, Mtaka ambaye ni mkuu wa wilaya ya Mvomelo, Morogoro, alishinda kwa kura 50 dhidi ya 29 za Ikangaa, Katibu Mkuu wa zamani wa shirikisho hilo wakati huo ikijulikama kama TAAA.
Mtaka alipata kura hizo katika kura za marudio baada ya raundi ya kwanza kukosekana mshindi wa moja kwa moja miongoni mwa wagombea wanne waliokuwa wamejitosa katika nafasi hiyo kwa Ikangaa kupata kura 25 na Mtaka kura 36.
Waliochemkia raundi ya kwanza ni Francis John aliyeambulia kura 15 na Henry Nyiti aliyepata kura 7,hivyo raundi ya pili kushudia ushindani mkali kati ya Ikangaa na Mtaka.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo majira ya saa 3:30 usiku, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi huo, Henry Tandau, alisema  kurudiwa kwa nafasi ya Rais na Katibu Mkuu, ilitokana na wagombea kushindwa kufikia asilimia iliyohitajika kwa mujibu wa kanuni.
Ushindani mwingine ulikuwa kwenye nafasi ya Katibu Mkuu iliyokuwa ikishindaniwa na watu wanne, akiwemo Suleiman Nyambui aliyekuwa akitetea, John Bayo, Zainab Mbiro na John Manyama, lakini Nyambui alishinda kwa kura 41 dhidi ya 38 za Bayo, katika raundi ya pili.
Wagombea wawili katika nafasi tofauti, Makamu wa Kwanza wa Rais (Utawala) ilikwenda kwa William Kallaghe, aliyekuwa mgombea pekee kwa kura 78.
Katika nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais (Ufundi), iliyokuwa ikiwaniwa na wagombea wawili, Dk. Hamad Ndee alishinda kwa kura 55, akimbwaga Herman Ndisa aliyepata kura 42.
Nafasi nyingine iliyokuwa na ushindani ni Katibu Mkuu Msaidizi , iliyokuwa ikiwaniwa na watu wanne, lakini Ombeni Zavalla akishinda kwa kura 40, Julius Murunya (32), Lucas Nkungu na Leonard Mandara, kila mmoja akipata tatu.
Nafasi ya Mweka Hazina ilikuwa na mgombea mmoja, Is- Haq Seleman, aliyepata ushindi wa kimbunga wa kura 78kati ya 79.
Mbali ya nafasi ya Rais na Katibu Mkuu, kivumbi kingine kilikuwa kwenye nafasi 10 za ujumbe wa shirikisho hilo, zilizokuwa zikiwaniwa na wanachama zaidi ya 30.
Hata hivyo, mhariri wa michezo wa gazeti la Tanzania Daima, Tullo Chambo, alifunga pazia la nafasi zilizokuwa zikiwania baada ya kupata kura 37, akiungana na Mwinga Mwanjala ( 53), Lwiza John (50), Peter Mwita ( 50), Zakaria Gwandu ( 47).,  Meta Petro Bare ( 46), Zakaria Barie (45), Rehama Killo( 42), Robert Kalyahe ( 41) na Christian Matembo (38).
                           

Post a Comment

Previous Post Next Post