Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa
2011/2012 kuwania ubingwa wa Tanzania Bara itafikia tamati Mei 5 mwaka huu kwa
bingwa kujulikana ambapo timu zote 14 siku hiyo zitakuwa uwanjani.
Klabu kongwe za mpira wa miguu nchini Simba
na Yanga zitakutanisha timu zao katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam. Nayo Oljoro JKT itakuwa mwenyeji wa Polisi Dodoma katika mchezo
utakaofanyika Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha na Ruvu Shooting
itacheza na Villa Squad katika Mabatini, Mlandizi.
Mechi nyingine zitakuwa kati ya Coastal
Union na Toto African itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, African
Lyon na JKT Ruvu (Uwanja wa Manungu, Morogoro), Azam na Kagera Sugar (Uwanja wa
Chamazi, Dar es Salaam) na Moro United na Mtibwa Sugar (Uwanja wa Jamhuri,
Morogoro).
Kwa mujibu wa kanuni namba
4(2)(c) ya Ligi Kuu ya Vodacom, timu tatu za mwisho katika msimamo wa ligi
zitashuka daraja. Tayari Moro United na Polisi Dodoma zimeshashuka, iliyobaki
itajulikana baada ya mechi za Jumamosi ambazo zote zitaanza saa 10 kamili
jioni.
MIKOA SITA YAOMBA UENYEJI
LIGI YA TAIFA
Mikoa sita imeshaomba kuwa
wenyeji wa Ligi ya Taifa itakayochezwa katika vituo vitatu tofauti. Ligi hiyo
inayoshirikisha mabingwa wa mikoa inatarajia kuanza baadaye mwezi
huu.
Kamati ya Mashindano ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inatarajia kukutana wakati wowote
kupitia maombi hayo kabla ya kufanya uamuzi wa vituo na tarehe ya kuanza ligi
hiyo.
Mikoa iliyoomba vituo ni Dar
es Salaam, Kigoma, Lindi, Mara, Shinyanga na Singida.
Boniface
Wambura
Ofisa
Habari
Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)