HALI ndani ya klabu ya Yanga imeendelea kuwa tete
baada ya jana wanachama kuutaka uongozi wa klabu hiyo chini ya Mwenyekiti wake
Lloyd Nchunga kuitisha mkutano mkuu wa wanachama kwa mujibu wa katiba.
Hatua hiyo inafuatia kesi iliyofunguliwa Septemba
4,2011 katika mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu
na wanachama Kingwaba Kingwaba, Juma Matimbwa na Siwema Chiokota kufutwa.
Akizungumza na mamapipiro blog leo, mmoja ya
wanachama wa klabu hiyo akiwakilisha kundi la vijana Bakili Mohammed Makele alisema
kwamba wamefikia hatua hiyo baada ya kuona mambo ndani ya klabu hiyo
yanaharibika hivyo mahala pa kupatikana jibu ni katika mkutano mkuu.
Alisema uongozi wa Nchunga umeshindwa kuitisha mkutano
huo kwa kivuli cha kusingizia uwepo wa amri hiyo ya mahakama kitu huku
akiambatana na baadhi ya wanachama mahakamani kushinikiza mkutano huo kuendelea
kusimamishwa, lakini ukweli ni kwamba
amri hiyo ililenga mkutano wa Septemba 4 tu.
Aliongeza pamoja na kutafuta mahala pa kuongelea
matatizo yao wanataka taarifa za mapato na matumizi ya klabu, masuala ya
mikataba na mambo mengineyo ambayo ni muhimu na wanachama wana haki ya
kuyafahamu.
“Tunachohitaji ni mkutano mkuu wa wanachama ili tupate
pa kusemea yanayotusibu, klabu yetu inaenda mrama, tunahitaji mapato na
matumizi na hata kujua mikataba waliyoingia viongozi,”alisema.
Makele aliongeza kuwa wanachama hawana mpango wa
kumuondoa madarakani Nchunga kama anavyohofia kwa sasa, kikubwa ni kufuata katiba ya Yanga na soka kwa ujumla na hasa
ikizingatiwa uongozi haujawahi kufanya mkutano tangu uingie madarakani mwaka
juzi.
Naye mwanachama Said Bakari alisema kuwa Nchunga
anadhalilisha taaluma ya Wanasheria kutokana na kutofuata katiba ya Yanga na
soka kwa ujumla katika kuongozi hivyo hana budi kushitakiwa hata kwa Shirikisho
la soka Tanzania (TFF) .
“Yanga imepoteza mwelekeo kutokana na viongozi
wachache kufanya mambo kinyume na katiba, hali hii mbaya sana na inazidi
kuipeleka pabaya klabu, tunaomba sana tena sana mwenyekiti wetu Nchunga aitishe
mkutano,”alisema Bakari.