KLABU ya Yanga imefanikiwa kunasa sahihi ya beki wa Simba Kelvin Yondan 'Vidic', kwa ajili ya
kuichezea timu hiyo katika msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Habari za uhakika zilizopatikana Dar es Salaam jana kutoka ndani ya Yanga, zilidai kwamba Yondan amesaini mkataba wa miaka miwili.
“Tayari tumeishasajili wachezaji wawili ambao ni Nizar Khalfan mwaka mmoja na Yondan, bado wengine watatu wakiwemo wa kigeni,” kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho kiliongeza kwamba mlinda mlango namba moja Yaw Berko, naye ameongezewa mkataba wa mwaka mmoja na wameondoka jana na mshambuliaji Keneth Asamoah kwenda kwao Ghana kwa ajili ya mapumziko.
Gazeti hili lilimtafuta Salum Rupia ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga kuelezea suala la usajili wa Yondan lakini hakupatikana baada ya simu yake ya mkononi kuita
bila majibu.
Aidha, alipotafutwa Mwenyekiti wa Yanga Lloyd Nchunga, alisema kwamba hahusiki na mambo ya usajili, mambo yote ya usajili aulizwe Rupia.
“Nisingependa kuzungumzia mambo ya usajili, mambo ya usajili muulizeni Rupia ndiye anajua,” alisema Nchunga.
Hata hivyo Nchunga kwa sasa yuko kwenye shinikizo ambapo wanachama wa klabu hiyo wanamtaka ajiuzulu kwa madai ya kushindwa kuiendesha klabu hiyo.
Yondani hakupatikana kuzungumzia, hilo kwa kuwa amesafiri na timu yake ya Simba Sudan na wanatarajiwa kurejea leo.
Kwa muda mrefu Yanga walikuwa wakimsaka Yondan bila mafanikio. Mchezaji huyo ameshawahi kuingia kwenye mgogoro wa mara kwa mara na mashabiki na viongozi wa Simba
wakidai kuwa ni mamluki wa watani wao hao wa jadi.
CHANZO:GAZETI LA HABARI LEO