KLABU ya soka ya Yanga imewapiga tena bao la kisigino
mahasimu wao wa jadi nchini Simba baada ya kumuongezea mkataba wa miaka
miwili nyota wake Jerryson Tegete.
Wakati ligi kuu soka Tanzania Bara ikielekea ukiongoni,
Simba ambao ni mabingwa wa ligi hiyo walianza mpango wa kutaka kumsajili
mchezaji huyo baada ya kuwepo taarifa kutoka Yanga kwamba haina mpango naye
tena.
Hata hivyo, baada ya tetesi za Simba kumuwania Tegete kuzagaa
mtaani ndipo Yanga iliporudi nyuma na kuamua kumfunga mchezaji huyo ambaye
mkataba wake ulikuwa unalizika mwezi huu hadi mwaka 2014.
Mmoja ya wadau wa
Yanga wanaohusika na usajili wa wachezaji katika klabu ya Yanga alisema jana
kwamba wameamua kumbakiza kundini Tegete kutokana na umuhimu alionao katika
kikosi hicho.
“Napenda niwatoe shaka wanayanga kwamba kwa Tegete
ataendelea kuvaa uzi wa njano na kijani kwa miaka miwili…wale walikuwa
wakimuwania nawapa pole kwani ameshamwaga wino jangwani,”alisema.
Tegete ambaye msimu
uliopita hakuweza kung’ara alitua Yanga
mwaka 2008, akitokea sekondari ya Makongo, ambapo kutokana na umahiri alionao
kwa nyakati tofauti alipata kuichezea timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
Yanga ambayo kwa sasa imeingia vita na Simba baada ya
kumsainisha mkataba wa miaka miwili nyota wake Kelvin Yondan ‘Vidic’, pia
imeshamsajili kipa wa Simba Ally
Mustafa ‘Barthez’ ikionekana kama kulipa kisasi baada ya Simba kumsajili Kiggi Makassy.