RAIS wa Shirikisho
la soka Tanzania (TFF) Leodger Tenga
amemwagia sifa kocha wa sasa wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mdenmark
Kim Poulsen kwamba ni mtu wa kazi na hajui anasa.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari jana katika ofisi za TFF jijini Dar es Salaam, Tenga
alisema kuwa kwa mwenendo huo, anamatumaini naye makubwa katika kukiletea
mafanikio kikosi hicho kwani akitoka
nyumbani kwake amekwenda sokoni au kazini na hajui baa wala sehemu za starehe.
Alisema kwamba
matumaini yao kwa Kim ni kutokana na timu yake ya sasa kuundwa na asilimia
kubwa ya vijana walio na wastani wa umri wa miaka 23 na kwamba hata wakubwa
wachache, rika la akina Juma Kaseja na Haruna Moshi ‘Boban’ wana miaka
isiyozidi 27.
Aliongeza
kuwa, kwa jitihada alizozionyesha hawana budi kumpongeza Kim na vijana wake kwa
ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Gambia, Jumapili katika mchezo wa kuwania tiketi
ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil na ameomba timu
hiyo iungwe mkono zaidi ili ifike mbali.
“Tumefika
hapa baada ya jitihada kubwa, ikiwemo kubadilisha kocha. Kupambana na nidhamu,
tulimuambia mwalimu, tafadhali, hakikisha nidhamu, utendaji na jitihada za
mazoezi, usiogope mchezaji, ita mchezaji, nampongeza sana na hakuna jambo la ajabu kwa sababu
tunamjua Kim, ni mtu wa kazi, mwaka mzima”alisema Tenga.
Tenga aliongeza
kuwa, tangu kocha huyo awasili mwaka
jana alianzisha programu nzuri ya vijana ambao amekuwa akiwakusanya kila mwezi
na kuwanoa jambo ambalo limesababisha hivi sasa awe na timu nzuri ya taifa,
baada ya kupandishwa kutoka kocha wa timu za vijana, hadi ya wakubwa, akirithi
mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Poulsen.
“Wale vijana
Sure Boy (Salum Abubakar) na Damayo (Frank) wamecheza pamoja karibu mwaka mzima
timu ya vijana chini ya Kim na wanaelewana sana . Sasa tumekwishaanza kuandaa utaratibu
wa kuwapatia vijana wataalamu wa saikolojia, ili wawafundishe mambo, namna ya
kuzungumza na Waandishi wa Habari, kuweza kujiami na kadhalika,”alisema
Taifa Stars
hivi sasa inashika nafasi ya pili katika Kundi C, kwa pointi zake tatu, mabao
mawili ya kufunga na matatu ya kufungwa, nyuma Ivory Coast inayoongoza kwa
pointi zake nne, mabao manne ya kufunga na mawili ya kufungwa, wakati Morocco
inashika nafasi ya tatu kwa pointi zake mbili, mabao matatu ya kufunga na
matatu ya kufungwa na Gambia yenye pointi moja, mabao mawili ya kufunga na
matatu ya kufungwa inashika mkia.
Stars
Jumapili itahamishia mawindo yake katika kinyang’anyiro cha tiketi ya kucheza
Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani Afrika Kusini kwa kumenyana na
Msumbiji mjini Maputo
na inatarajiwa kuondoka nchini Ijumaa. Katika mchezo wa kwanza, timu hizo
zilitoka sare ya 1-1 Dar es Salaam
na Stars inatakiwa lazima kushinda ugenini ili kuitoa Mambas na kusonga mbele.