CHEKA KUMKABILI NYILAWILA JULAI 29,PST KUSIMAMIA PAMBANO


BONDIA Francis Cheka atapanda ulingoni Julai 29 kuwania ubingwa wa mabara dhidi ya Karama Nyilawila kwenye ukumbi wa PTA pambano hilo likiwa linasimamiwa na Chama cha Ngumi za kulipwa nchini (PST).
Akizungumza jijini jana mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni ya Afrika Kabisa Entertaiment ambao ni  mratibu wa pambano hilo Osward Mlay 'Makele' alisema mkanda huo upo wazi  hivyo mahasimu hao watapambana ukizingati wanakaribiana pointi na kwamba pambano hilo litakuwa la uzito wa Kg76.
Alisema pambano hilo ambalo linavuta hisia za mashabiki wengi wa ngumi litakuwa na mapambano sita ya utangulizi ambapo Seba Temba  atamenyana na Stam Kessi kg 66 wakati Cosmas  Cheka atapimana nguvu na Fadhili Hawazi kg 62 huku Juma Kihiyo akicheza na  Ibrahimu Mahokola kg 70.
Pambano lingine litawakutanisha bondia Hassan Kidebe dhidi ya Deo Samweli kg 57 wakati Antony Mathias atamenyana na Shaban  Kilumbe kg 54 na Amos Mwamakula atacheza na Sadick Momba uzito wa kg 60
Wakizungumzia pambano hilo mabondia hao walijitamba kila mmoja kuhakikisha atashinda na kutwaa mkanda huo.
Francis Cheka alisema " Karama ni bondia ninayemkubali kuliko mabondia wote na ninamuhofia, mashabiki wangu naomba wakubali matokeo yoyote katika hili pambano kunakushinda na kushindwa lakini lengo langu ni kushinda kwani nilishampiga mara nyingi tu.
"Nitaendeleza uteja wa mabondia wa Dar es Salaam ambao kazi yao wamekaa kusema natumia ndumba, nawambia kabisa hakuna ushirikina katika ngumi, ni mazoezi tu, wakiendelea kushiriki uchawi ipo siku watapigwa vibaya na nitaendelea kuwapiga mpaka wajue kufanya mazoezi ya nguvu."alijinasibu Cheka
Kwa upande wa Nyilawila  alisema "Najua Cheka anafanya mazoezi magumu lakini hatotoka ulingoni itakuwa mwisho wake, na aache kukimbia kimbia ulingoni ajitoe mhanga tupigane na waamuzi wawe  makini wasipendelee."alisema Karama na kudai kuwa atampiga Cheka na kumbikiza kama 'pepo',anavyotolewa kwa nguvu za Mungu.
mwisho

Post a Comment

Previous Post Next Post