Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeridhia ombi la Chama cha Mpira
wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam
(DRFA) kuanza mchakato wa uchaguzi wake Julai 15 mwaka huu.
DRFA iliwasilisha ombi TFF ili kusogeza mbele kuanza kwa mchakato
huo kwa vile Katiba yao
ambayo waliagizwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuifanyia marekebisho kabla ya
kuingia kwenye uchaguzi huo bado iko kwa Msajili.
Awali DRFA ilikuwa ianze mchakato wa uchaguzi Julai Mosi
mwaka huu. Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, mchakato wa
uchaguzi unatakiwa kuchukua siku 40 tangu kuanza kutolewa fomu kwa wagombea
hadi siku yenyewe ya uchaguzi.
Pia Kamati ya Uchaguzi ya TFF imekubali ombi la Chama cha
Mpira wa Miguu Mkoa wa Kigoma (KRFA) kuanza mapema mchakato wa uchaguzi wake.
Sasa mchakato wa uchaguzi wa chama hicho utaanza Septemba Mosi mwaka huu badala
ya Septemba 15 mwaka huu kama ilivyokuwa
imepangwa awali.