Kocha mkuu wa Yanga Tom Saintfiet akizungumza na waandishi wa habari leo wakati akitaja kikosi cha wachezaji wa timu hiyo watakaoshiriki michuano ya Kagame, kushoto ni kaimu meneja wa bia ya Kilimanjaro Oscar Shelukindo na kulia ni Katibu Mkuu wa Yanga, Mwesiga Selestine.
WAKATI michuano ya kombe la
Kagame ikitarajiwa kuanza kutimua vumbi kesho, kocha mkuu wa mabingwa watetezi
wa michuano hiyo, Mbelgiji Tom Saintfiet ametangaza silaha atakazotumia katika
michuano hiyo huku akimuengua nahodha wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’ .
Saintfiet pia amewaacha
kwenye kikosi hicho wachezaji nyota chipukizi watatu wakiwemo Simon Msuva,
Omega Seme na Frank Damayo.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam leo, Saintfiet pamoja na kumsifu Nsajigwa kuwa ni mchezaji mzuri na muhimu,
alisema ameamua tu kutomjumuisha katika michuano hiyo badala yake atamtumia katika Ligi Kuu soka Tanzania Bara.
Kuhusiana na wachezaji
chipukizi, kocha huyo alisema watakuwa
na majukumu ya kitaifa na timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 20
inayojiandaa na mchezo wake wa kufuzu fainali za mataifa ya Afrika dhidi ya
Nigeria, itakayopigwa Julai 29.
“Kanuni zinanitaka kuachia
wachezaji siku tano kabla ya mechi na hawa vijana watarudiana na Rwanda
Jumatatu kabla ya kuanza kujiandaa na mechi yao na Nigeria…nasikitika kutokuwa
nao lakini sina jinsi,”alisema.
Kocha huyo ambaye ameteua
wachezaji kwa kushirikiana na wasaidizi wake Fred Felix Minziro na Mfaume
Athuman, pia amewaacha katika kikosi xchake wachezaji nyota kama Nurdin Bakari
na Salum Telela kutokana na kukabiliwa na majeruhi.
Akizungumzia michuano hiyo,
Sainfiet alisema ni migumu kwani timu nyingi zinazoshiriki zimetoka katika Ligi
tofati na Yanga ambayo ilikuwa mapumziko kwa muda mrefu na kuanza mazoezi hivi
karibuni lakini anaimani na kikosi chake.
“Kwa siku chache nilichokuwa
nancho nimebainia vipaji na hata mchezo wetu wa kirafiki na JKT Ruvu Jumanne
wachezaji walitimiza wajibu wao ipasavyo hivyo nataraji mambo mazuri zaidi
katika Kagame,”alisema.
Kocha huyo aliongeza kuwa ana
imani kubwa na wachezaji wake kwani pia wana nindhamu ya ndani na nje ya uwanja,
hivyo ana uhakika wataweza kushinda mataji muhimu ambayo waliyakosa mwaka jana.
Aliongeza kuwa, Yanga
inahitajki kushinda mchezo wake wa kwanza dhidi ya Atletico na hivyo kujiweka
katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
Aliwataja wachezaji hao ni
pamoja na makipa Yaw Berko na Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Juma Abdul, David
Luhende, Kelvin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Godfrey Taita, Ladislaus
Mbogo, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika.
Kwa upande wa viungo ni
pamoja na Athumani Iddi ‘Chuji’, Rashid Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’, Haruna
Niyonzima, Shamte Ally, Nizar Khalfan, Idrisa Assenga, Hamisi Kiiza na
washambuliaji Said Bahanuzi na Jerry Tegete.
Naye kaimu meneja wa bia ya
Kilimanjaro inayozidhamini timu za Simba na Yanga, Oscar Shelukindo alisema kampuni ya bia
Tanzania (TBL) itaendelea kuwa bega kwa bega na timu hizo Simba katika
kuhakikisha inashiriki kikamilifu mashindano hayo.
Shelukindo amezitaka timu
hizo kujibidiisha ili kuhakikisha zinalibakisha kombe hilo hapa nchini ambapo
Yanga itaanza kampeni hiyo kesho kwa kukwaanza na Atletico ya Burundi, huku
Simba itaianza Jumapili kwa kukwaana na URA ya Uganda.
Mbali na Simba na Yanga, michuano hiyo pia
itashirikisha timu za Azam Fc, Mafunzo ya Zanzibar APR ya Rwanda, El Salam Wau ya Sudan Kusini, Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo
(DRC) na Ports ya Djibouti