Msanii wa Ras Innocent Nganyagwa
akiwasilisha mada kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii. Kushoto kwake ni Afisa
Habari Mkuu BASATA Bi Agnes Kimwaga.
Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari kutoka Baraza la Sanaa
la Taifa (BASATA) Godfrey Lebejo akisisitiza jambo wakati akihitimisha programu
ya Jukwaa la Sanaa wiki hii.
Na Mwandishi Wetu
Watanzania wametakiwa kuuenzi
utamaduni wa makabila ambao una thamani kubwa sana, wito huu umetolewa wiki hii
kwenye ukumbi wa BASATA na mwanamuziki mkongwe wa regge nchini na mtafiti
mbobevu wa masuala ya historia za jamii, Innocent Nganyagwa, alipokuwa akiwasilisha mada katika Jukwaa la
Sanaa kuhusu Umuhimu wa
Utafiti Wa Makabila Katika Kuendeleza Utamaduni Wetu.
Alisema tamaduni za makabila mengi
ya Tanzania
zina mashiko mazuri na yenye thamani ambayo yakienziwa na kuendelezwa,
yatawasidia watu katika maendeleo ya sasa.
Alisema Watanzania tunapaswa
kujitambua na kujua mashiko ya Sanaa na tamaduni zetu na kuhuisha thamani ya
maadili yetu kitaifa.
“Kila kabila lilikuwa na taratibu
zake na mifumo yake ya utawala na shughuli zake za uchumi, pia makabila
mbalimbali yalishirikiana, mambo haya yakiendelezwa ni dhahiri tunaweza
kuendela zaidi katika zama za sasa za changamoto za utandawazi, uliorahisisha
maendeleo lakini pia ukatuletea baadhi ya tamaduni za kigeni zinazopotosha
maadili.
Msanii huyu aliwataka Watanzania
kufanya tafiti zaidi na kujitambua wao ni nani na asili yao ni nini ili
wasitegemee historia zilizoandikwa na wageni peke yake, kwani nyingi zinaishia
katika mazungumzo waliyopewa bila kushiriki kikamilifu katika kupata taarifa
zaidi za historia hizo kwa kuzipima katika ‘mzania jumuishi’ wenye kina kirefu
cha mila na desturi.
Nae Kaimu Katibu
Mtendaji wa BASATA, ndugu Lebejo, alisistiza kuwa tungeendeleza kilichopo kwenye
tamaduni zetu na kukichanganya na teknolojia tungefika mbali sana katika kila
eneo, tushikilie mila zetu tusiige vya Wazungu kwani wao wana mila zao na
wanaziendeleza kwa mujibu wa mashiko yao ya utamaduni wao, tusibweteke na
kupenda vya kuiga vya kigeni wakati tuna mambo yetu mengi yenye thamani na
mafundisho ya kuishi maisha sadifu ya kimaadili.
“Tujitambue na kuzifahamu
mila zetu kwa kufanya tafiti, tusisubiri mpaka tuwe maprofesa ili kuweza
kufahamu tulikotoka, kwani mengi kati ya yanayohusu utamaduni wetu yanatuzunguka
katika maisha yetu ya kila siku. Ni suala tu la kuwa na mtazamo chanya na
kuamua kwa dhati kuuenzi utamaduni wetu”,alisisitiza ndugu Lebejo.
Kweli aiyethamini utamaduni wake ni mtumwa wa utamaduni wa wenzake anaouthamini
ReplyDelete