TIMU ya soka ya JKT Ruvu jana imefanikiwa kutwaa ubingwa wa
ligi maalum wa timu za majeshi zinazorajiwa kushiriki ligi kuu soka Tanzania
Bara msimu wa 2012/2013 iliyokuwa ikifanyika kwenye uwanja wa Mabatini uliopo
Mlandizi, Pwani.
JKT ilitwaa ubingwa huo kutokana na kufikisha pointi 9
ilizozipata kupitia michezo yake mitano ya ligi hiyo iliyoanza kutimua vumbi
Agosti 15 mwaka huu na kushirikisha timu 6.
Kwa ushindi huo, maafande hao walikabidhiwa kombe kubwa
pamoja na fedha taslimu sh 100,000 kutoka kwa mgeni rasmi katika fainali hizo
Hassan Othman ‘Hassanoo’ ambaye ni mwenyekiti wa chama cha soka mkoa wa Pwani
(COREFA).
Oljoro JKT ilishika nafasi ya pili kwa kufikisha pointi 9
pia, Mgambo ilishika nafasi ya tatu kwa pointi sita, Ruvu Shooting ilishika
nafasi ya nne kwa kuwa na pointi sita, wakati polisi Dar es Salaam ilishika
nafasi ya tano kwa pointi sita na
African Lyon ambayo ilikuwa timu mwalikwa ilishika mkia kwa kuwa na pointi
tatu.
Mshambuliaji wa maafande wa JKT Oljoro Paul Nonga aliibuka
kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo.