Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuanzia msimu huu wa 2012/2013 itakuwa na timu 24 kutokana na mabadiliko ya mfumo wa mashindano yaliyofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kamati ya Utendaji ya TFF ilikutana Julai 29 mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine ilifanya mabadiliko ya mfumo wa mashindano ikiwemo FDL kuchezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini badala ya ule wa awali wa vituo.
Kutokana na mabadiliko hayo, timu za FDL zitagawanywa katika makundi mawili ya timu 12 kila moja kutokana na ukaribu wa kanda na kucheza kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.
Timu ya kwanza kutoka kila kundi itapanda kucheza Ligi Kuu msimu unaofuata wakati ya tatu itakayoungana na hizo mbili itapatikana kwa mechi za nyumbani na ugenini kwa timu zilizoshika nafasi ya pili katika kila kundi.
Ili kufikisha idadi ya timu 24 kwenye FDL, Kamati ya Utendaji ya TFF kwa kuzingatia mapendekezo ya Kamati ya Mashindano imeamua timu tatu za juu kwenye Ligi ya Taifa kutoka vituo vyote vitatu vya ligi hiyo zimepanda daraja.
Sasa timu 24 za FDL ni Ashanti United (Dar es Salaam), Burkina Moro (Morogoro), Green Warriors (Dar es Salaam), Kanembwa JKT (Kigoma), Kurugenzi Mafinga (Iringa), Majimaji (Ruvuma), Mbeya City (Mbeya), Mkamba Rangers (Morogoro), Mlale JKT (Ruvuma) na Morani (Manyara).
Nyingine ni Moro United (Dar es Salaam), Mwadui (Shinyanga), Ndanda (Mtwara), Pamba (Mwanza), Polisi (Arusha), Polisi (Dodoma), Polisi (Iringa), Polisi (Mara), Polisi (Tabora), Rhino Rangers (Tabora), Small Kids (Rukwa), Tessema (Dar es Salaam), Transit Camp (Dar es Salaam), Villa Squad (Dar es Salaam).
Timu nne zitashuka daraja kurudi Ligi ya Mkoa. Timu hizo ni mbili zilizoshika nafasi za mwisho kwa kila kundi. Timu nne zitakazopanda kucheza FDL zitapatikana kwa mchujo utakaohusisha mabingwa wa mikoa.
Kwa mfumo huo mpya wa mashindano, ligi za mikoa zitakazosimamiwa na kuendeshwa na vyama vya mpira wa miguu vya mikoa zinatakiwa kuwa na timu zisizopungua 16 na zisizozidi 20. Ligi za mikoa pia zitachezwa mwaka mzima kwa mikondo miwili (nyumbani na ugenini).
Ligi ya mkoa itashusha timu mbili na kupandisha nyingine mbili kutoka ligi ya wilaya. Ligi za wilaya zitakazosimamiwa na kuendeshwa na vyama vya mpira wa miguu vya wilaya zinatakiwa kuwa na timu zisizopungua 10 na zisizozidi 20.
Kwa wilaya zenye timu zaidi ya 20, chama husika cha mpira wa miguu kitapanga utaratibu wa kuzichuja kwa mashindano ili kupata zile bora 20 zitakazocheza ligi rasmi ya wilaya.
Mabingwa wa wilaya katika mkoa husika watacheza mechi za kuchujana (play offs) ili kupata timu mbili zitakazopanda daraja kucheza ligi ya mkoa husika.
Kutokana na mabadiliko hayo ya mfumo wa mashindano, sasa madaraja rasmi ya ligi ni Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi ya Mkoa (Ligi Daraja la Tatu) na Ligi ya Wilaya (Ligi Daraja la Nne).
TFF inasisitiza kuwa kwa mujibu wa kalenda yake ya matukio, kipindi cha usajili wa wachezaji kwa madaraja yote ni kimoja, na ligi zitachezwa kwa wakati mmoja.
Usajili wa hatua ya kwanza ni kuanzia Juni 15 hadi Agosti 10 mwaka huu wakati kipindi cha pili cha usajili ni Agosti 21 hadi Septemba 4 mwaka huu. Usajili wa dirisha dogo ni Novemba 15 hadi Desemba 15 mwaka huu.
Ligi kwa madaraja yote zitaanza Septemba. Ligi Kuu itaanza Septemba Mosi mwaka huu, Ligi Daraja la Kwanza ni Septemba 15 mwaka huu, Ligi ya Mkoa na ile ya Wilaya zenyewe zitaanza Septemba 8 mwaka huu.
Mechi za kufungua msimu kwa madaraja yote (Ngao ya Jamii) ambazo kwa sasa zinakutanisha bingwa na makamu bingwa zitachezwa Agosti 25 mwaka huu wakati michuano ya Kombe la FA itaanzia wilayani Septemba 24 mwaka huu.