MSONDO KUBEBA JENERETA KATIKA PAMBANO LAO NA SIKINDE IDD MOSI


Na Mwandishi Wetu
Ili kuepukana na hujuma ambazo zinaweza kutokea kwenye mpambano wao, bendi ya Msondo Ngoma itatumia jenereta dhidi ya mahasimu wao wa jadi Mlimani Park Orchestra “Wana Sikinde” utakaofanyika siku ya Iddi Mosi katika viwanja vya Leaders Club, Kinondoni.
Meneja wa bendi hiyo, Said Kibiriti, amesema wameamua kufanya hivyo ili kuepuka hujuma ambazo zinaweza kufanywa na wapenzi wa wapinzani wao ya kukata umeme na kama ilivyotokea kwenye pambano la Desemba 25 mwaka jana.
“Tunakumbuka sana kwenye pambano letu lililopita wakati wa Krismasi mwaka jana pale TCC Club Chang’ombe, wapenzi wa Sikinde walitukatia umeme kwa makusudi ili tukose ushindi,” alisema Kibiriti.
Alisema kwa kuepuka hilo watatumia genereta kubwa kuanzia mwanzo wa shindano hadi mwisho.
Amewatoa wasiwasi wapenzi wa Msondo kuwa jenereta hilo ni kubwa na lenye uwezo wa kuwasha hata kijiji kizima, hivyo hata kiwango cha muziki utakaopigwa utakuwa mkubwa. “Jenereta letu litakuwa chini ya ulinzi mkali ili kuepuka usumbufu,” alisema Kibiriti.
Kwenye pambano la mwaka jana, Msondo ilitumia umeme wa kawaida ambao ulikuwa ukikatika mara kwa mara, kitu ambacho kilidaiwa kuwa ni hujuma kutoka kwa wapenzi wa Sikinde ambao wao walikuwa wanatumia umeme wa jenereta.
Pambano la Msondo na Sikinde tayari limeanza kuvuta hisia za mashabiki wa muziki wa dansi nchini ambao wanatarajia kumiminika kwa wingi siku ya Iddi Mosi kwenda kushuhudia mpambano huo iliyodhaminiwa na kinywaji cha Konyagi.

Post a Comment

Previous Post Next Post