Ngorongoro Heroes, timu ya
Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 imewasili asubuhi hii (Agosti 10
mwaka huu) kwa ndege ya Overland Airways kwenye mji wa Ilorin ,
Jimbo la Kwara lililo Kusini mwa Nigeria tayari kwa mechi ya
marudiano dhidi ya wenyeji Flying Eagles itakayochezwa Jumapili.
Mechi hiyo ya raundi ya pili
ya michuano ya U20 ya Afrika itachezwa kwenye Uwanja wa Township kuanzia saa 10
kamili jioni kwa saa hapa ambapo Tanzania itakuwa ni saa 12 kamili
jioni. Ngorongoro Heroes ilitua jana (Agosti 9 mwaka huu) jijini Lagos ambapo ililala
kabla ya kuja hapa.
Msafara wa Ngorongoro Heroes
wenye watu 27 ukiongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA) ulipokea na Ofisa Ubalozi wa Tanzania nchini Nigeria,
Jones Mndeme na viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nigeria (NFF) umefikia
hoteli ya Kingstone Grand Suites.
Kwa mujibu wa Kocha wa
Ngorongoro Heroes, Jakob Michelsen, timu itafanya mazoezi leo jioni (Agosti 10
mwaka huu) wakati mazoezi ya mwisho yatakuwa kesho jioni (Agosti 11 mwaka huu)
kwenye uwanja ambao utatumika kwa mechi ya Jumapili.
Wachezaji wote wako katika
hali nzuri isipokuwa Issa Rashid na Aishi Manula ambao walikuwa wakisumbuliwa
na tumbo baada ya timu kufika jana (Agosti 9 mwaka huu) jijini Nairobi ,
Kenya ambapo ilibadili ndege
kuja Nigeria .
Hata hivyo, hali zao zinaendelea vizuri na huenda wakawa sehemu ya kikosi cha
kwanza kitakachoivaa Flying Eagles.
Mbali ya Rashid na Manula,
wachezaji wengine walioko hapa kwenye kikosi cha Ngorongoro Heroes ni Barwany
Khomeiny, Samir Ruhava, Dizana Yarouk, Leonard Muyinga, Hassan Ramadhan, Jamal
Mroki, Omari Kheri, Frank Domayo, nahodha Omega Seme, Abdallah Kilala, Hassan Dilunga,
Ramadhan Singano, Simon Msuva, Said Zege, Atupele Gren na Ramadhan Salum.
Mbali ya Michelsen, Benchi la
Ufundi linaundwa na Mohamed Rishad 'Adolf' (Kocha Msaidizi), Peter Manyika
(Kocha wa makipa), Nassoro Matuzya (Daktari), Joakim Mshanga (Physio), Juma
Kizwezwe (Mtunza vifaa) na Meneja wa timu John Lyimo.
Flying Eagles ambayo
ilishinda mechi ya kwanza mabao 2-1 nayo tayari imeshaingia hapa Ilorin ikitokea Lagos kwa
mechi hiyo ambayo matokeo yake yataamua timu ipi itaingia raundi ya tatu ambayo
ni ya mwisho kabla ya fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20
zitakazofanyika mwakani nchini Algeria .
Timu itakayovuka itacheza raundi hiyo na mshindi kati ya Congo Brazzavile na
Afrika Kusini.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF)
Ilorin, Kwara State, Nigeria
+2347068557566