NYOTA wa kimataifa wa Simba, Mganda Emmanuel Okwi ataendelea kubaki kwao
Uganda baada ya Shirikisho la Soka la nchi hiyo, FUFA, kuwaandikia Wekundu wa
Msimbazi, barua kumuomba aendelee kuwepo huko.
Awali, Okwi ambaye alikuwa kwao kuitumikia timu ya taifa, The Cranes
katika mechi yao ya kirafiki ya kalenda ya FIFA dhidi ya Malawi, ilikuwa arejee
nchini Jumapili kujiunga na wenzake waliopo kambini jijini Arusha.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema jijini Dar es Salaam
jana kwamba, FUFA imemtaka Okwi aendelee kubaki Uganda na wenzake, kwani wanatarajia
kucheza na Botswana Agosti 26.
Alisema, mbali ya Okwi, mchezaji mwingine wa kimataifa wa timu hiyo,
Mussa Mude, pia wa Uganda ambaye alikuwa majeruhi, hali yake imetengemaa na
kufikia mwisho wa mwezi huu, atakuwa ameshajiunga na wenzake.
Katika hatua nyingine, Kamwaga alisema kutokana na kusogezwa mbele kwa
Ligi Kuu bara, Simba itaendelea kujichimbia Arusha hadi Septemba 8 itakaporejea
jijini Dar es Salam kwa ajili ya mechi yake ya kuwania Ngao ya Hisani dhidi ya
Azam FC.