WAKATI timu zote za Ligi Kuu
Bara zikiwasilisha usajili wao, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema Kamati
yake ya Sheria, Katiba na Haki za Wachezaji chini ya Mwenyekiti wake Alex
Mgongolwa, ndiyo itakayotoa uamuzi juu ya utata wa wachezaji Ramadhan Chombo
‘Redondo’ na Kelvin Yondan.
Hatua hiyo inatokana na
majina ya wachezaji hao kupelekwa na timu mbili tofauti ambako Redondo
aliyekuwa akiichezea Azam msimu uliyopita, jina lake limeorodheshwa
pia na Simba huku Yondani aliyekuwa kwa Wekundu wa Msimbazi ameorodheshwa
kwenye kikosi cha Yanga.
Akizungumza na Waandishi wa
Habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema
kamati hiyo inatarajiwa kuketi Agosti 23 na 24 kupitia usajili wa wachezaji wa
klabu za Ligi Kuu Bara na Ligi Daraja la Kwanza, ambako zoezi hilo lilifungwa
juzi saa sita usiku.
Alisema, kuhusiana na
Yondani, Simba imewasilisha mkataba wake tu bila ya kuwemo kwenye fomu mama ya
klabu hiyo, huku Redondo jina likishindwa kuorodheshwa katika fomu mama ya Azam
Fc na pia kukosekana baadhi ya vielelezo, pamoja na mkataba wake ambao unaishia
Juni mwakani.
Osiah aliongeza kuwa,
ukiachana na hilo, timu zote 14 zitakazoshiriki ligi hiyo itakayoanza Septemba
Mosi mwaka huu, ziliwasilisha fomu huku Toto African ya Mwanza ikiwa ya mwisho
kufanya hivyo, baada ya kupata tabu katika kusajili kwa njia ya kompyuta kabla
ya TFF kuipa ushirikiano.
Alisema, kwa upande wa timu
za daraja la kwanza ni timu tano tu kati ya 24 zilizowasilisha usajili wake na
kuwa, huenda hali hiyo inatokana na mchakato wa kusajili kwa kompyuta
kuwatatiza wengi.
Aliongeza kuwa, kutokana na
hali hiyo, wameiagiza Kamati ya Mgongolwa, kukutana haraka ili kuangalia jinsi
ya kufanya kwani kanuni zipo kimya juu ya hilo .
Osiah alizitaja timu za
Daraja la Kwanza zilizowasilisha usajili ni
Polisi Dar Central, Taseme, Mkamba Rangers Fc, Transit Camp na Moro United.