SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF) limeeleza
kufurahishwa na hamasa iliyoko katika usajili hapa nchini.
Hayo yalisemwa jana na Rais wa TFF, Leodger Tenga alipozungumza na wahariri wa michezo wa vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Hata hivyo, Tenga alikosoa watu
wasio wataalamu wa ufundi kuendesha zoezi hilo, badala ya makocha au kamati za
ufundi.
Alisema walikubaliana kuruhusu usajili wa nyota
kutoka nje kwa lengo la kuhamasisha ushindani hapa nchini, kwani njia nzuri ya
kumpa ujuzi mchezaji ni kumpa nafasi kucheza na yule aliye mzuri zaidi.
“Utamaduni duniani kote, usajili unafanywa na
kocha, lakini hapa mchezaji anasajiliwa na mdhamini au kiongozi, mambo ambayo
hujiingiza kwenye matatizo, timu ikifungwa wanachama wanakufuata nyumbani. Mi
huwa nashangaa timu ikifungwa watu wanavamia viongozi, kumbe hatujajiweka
vizuri,” alisema.
Tenga alitaka wataalamu ndio wapewe jukumu hilo,
huku akisisitiza kuwa, vijana wenye vipaji ambao wapo hivi sasa hapa nchini
wapewe nafasi na si lazima kukimbilia nje, labda iwe kwa mchezaji mzuri zaidi.