RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF),
Leodegar Tenga, amewaomba radhi waandishi wa habari kutokana na adha waliyoipata
wakati wa fainali za Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam hivi karibuni.
Kutokana na tukio hilo, ambalo Waandishi
walizuiwa kuingia kwenye uzio wa Uwanja huo kufanya mahojiano mara baada ya
kumalizika kwa mechi ya fainali kati ya Yanga na Azam FC, ambako baadhi yao
walinyanyaswa kwa namna moja ama nyingine.
Akizungumza na Wahariri wa Michezo kwenye makao
makuu ya TFF jana, Tenga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya
Michezo Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, (CECAFA), alisema, yeye ni muumini
wa haki, hivyo amesikitishwa na hali iliyojitokeza, hivyo anaomba radhi na
asingependa hali hiyo iendelee tena.
“Mimi ni muumini wa haki, nawaomba radhi na
kuwapa pole wale waliopata misukosuko siku ile, sioni kwanini hili linajitokeza.
Nikiwa Rais wa TFF na Mwenyekiti wa CECAFA nawaomba radhi, halileti ‘image’
nzuri, hata kama kulikuwa na kuna kuelekzana lakini si kwa hali hii,” alisema
Tenga.
Tenga aliwataka viongozi wa TFF, Katibu Mkuu na
Ofisa Habari, kukutana na viongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo
Tanzania (TASWA), kukutana kujadili hali hiyo na kuweka mambo sawa ili isije
tokea tena huku akisisitiza, njia ya majadiliano ndio muafaka wakati wote.
Awali kutokana
na mtafaruku huo, TASWA ilitangaza mgogoro na kufikia uamuzi wa kususia
masuala yote yanayolihusu baraza hilo.