SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema
litaanza kufanyia kazi kwa vitendo tatizo la utumiaji wa dawa za kulevya
hususan bangi unaodaiwa kufanywa na baadhi ya wachezaji hapa nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Rais wa
TFF, Leodegar Tenga, alisema miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakabili ni
kile kinachodaiwa kuwa baadhi ya wachezaji wanatumia bangi, ingawa bado
hawajapata ushahidi.
“Tunasikia, lakini hatuna ushahidi, kwamba vijana
wetu wanatafuna bangi, ila viongozi wengi wamekuwa wakilisemea pembeni, sisi
kama wazazi jukumu letu ni kuwaelimisha juu ya athari zake, maana wao
wanaotumia wanaweza kuona inawaongezea hamasa, lakini hawajui madhara yake,”
alisema Tenga.
Alisema wameagiza suala hilo lianze kufanyiwa
kazi katika timu ya taifa, Taifa Stars na Ligi Kuu Bara, ambako viongozi
wanapaswa kukaa chini na vijana wao kuwapa elimu nasaha, kabla ya kuanza
kuchukuliwa hatua.
“Bangi na mpira ni vitu viwili tofauti, tumeagiza
elimu ianze kutolewa kuanzia national team (timu ya taifa) na Premier League
(Ligi Kuu), ikiwezekana waletewe hata wataalamu waweze kuwapa elimu kabla
hatujaanza kuchukua hatua, ambapo kutakuwa na testing (vipimo) ya kushtukiza na
atakayekataa, kanuni zinachukua mkondo wake mara moja,” alisisitiza Tenga.
Tenga aliongeza kuwa, suala hilo litawekwa katika
kanuni za Ligi Kuu na tayari Kamati ya Tiba imepewa maelekezo kuhusiana na
hilo, ambapo litaanza kufanyiwa kazi mara tu elimu itakapokuwa imetolewa kwa
walengwa.
Jumamosi iliyopita, Waziri wa Habari, Utamaduni
na Michezo, Dk. Fenera Mukangara pia aliwataka wachezaji chipukizi kutojiingiza
katika utumiaji wa dawa za kulevya wakati akitoa zawadi kwa washindi wa
michuano ya BancABC SUP8R, ambapo Simba walitwaa ubingwa.