Hassanoo
Aveva kulia akiwa na mwenyekiti wa Taswa, Juma Pinto
WANACHAMA maarufu wa klabu ya soka ya Simba, Evance Aveva
na Hassan Othaman ‘Hassanoo’ wamejitosa kuwania Uenyekiti wa vyama vya soka vya
mikoa ya Dar es Salaam (DRFA) na Pwani (COREFA).
Wakati Aveva akirejesha fomu ya kuwania uenyekiti wa
DRFA, Hassanoo amechukua fomu ya kutetea nafasi yake ya Uenyekiti Corefa,
katika uchaguzi utakaofanyika mwezi ujao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Aveva ambaye
aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Simba, alisema ameamua kuwania nafasi hiyo
ili kutimiza wajibu wake kama mwana michezo mwenye sifa zinazostahili kuongoza
chama chochote cha michezo.
Aveva aliongeza kuwa sababu ya kugombea kwake uongozi ni
kutaka kuleta mabadiliko katika chama hicho ambapo kwa kushirikiana na viongozi
wenzake iwapo atachaguliwa kukiongoza ana imani kutapatikana mafanikio makubwa.
“Kila mtu ananifahamu mimi kuwa ni mmoja ya wanamichezo
wa muda mrefu, pia utendaji wangu wa kazi…nadhani nitaweka wazi mikakati yangu
muda wa kampeni utakapofika,”alisema Aveva.
Naye Hassanoo alisema amelazimika kutaka kutetea tena
nafasi yake hiyo ili kuendeleza mikakati waliyoianzisha ambapo kwa asilimia
kubwa uongozi wake umetimiza uliyoahidi hivyo ni nafasi nyingine tena ya
kuufanyia mambo makubwa mkoa wa Pwani.