KOZI ya wakufunzi wa waamuzi (Futuro III Refereeing
Course) ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) inatarajiwa kuanza kesho kwenye hoteli ya
Holiday Inn jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la soka Tanzania
(TFF) Boniface Wambura, kozi hiyo itakayoanza saa tatu asubuhi itashirikisha jumla
ya washiriki 69 kutoka nchi 21 za Afrika.
Alisema kozi hiyo inayotarajiwa kumalizika Septemba 22
mwaka huu inafanyika katika maeneo mawili ya ufundi (technical) na utimamu wa
mwili (fitness).
Alizitaja nchi washiriki ni Afrika Kusini, Botswana,
Eritrea, Ethiopia, Gambia, Ghana, Kenya, Lesotho, Liberia, Malawi, Mauritius,
Namibia, Nigeria, Seychelles, Sierra Leone, Somalia, Swaziland, Tanzania,
Uganda, Zambia na Zimbabwe.
“Washiriki kutoka Tanzania kwenye kozi hiyo ni Joan
Minja, Leslie Liunda na Soud Abdi (technical) na Riziki Majalla (fitness),”alisema.
Wambura alisema kwamba
baadhi ya wakufunzi wa kozi hiyo wanaotoka FIFA na Shirikisho la soka Afrika
(CAF) ni Carlos Henriques anatoka Afrika Kusini, Fernando Gracia (Hispania),
Steve Bennett (Uingereza), Tarek Bouchamaoui (Tunisia), James Sekajugo
(Uganda), Bester Kalombo (Malawi), Felix Tangawarima (Zimbabwe) na An-Yan Lim
Kee Chong (Mauritius).
Aidha, Wambura alisema kozi hiyo itafunguliwa na Rais wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), mjumbe wa
Kamati ya Utendaji ya CAF na mjumbe wa Kamati ya Vyama (Associations Committee)
ya FIFA.