TIMU ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17
(Serengeti Boys) inaendelea vizuri na kambi ya mazoezi mkoani Mbeya ambapo
tayari imecheza mechi moja ya kujipima nguvu.
Kwa mujibu wa Ofisa habari wa Shirikisho la soka Tanzania
(TFF), Serengeti Boys jana ilikwaana na Tanzania
Prisons iliyoko Ligi Kuu ya Vodacom kwenye mji wa Nakonde ulioko mpakani mwa
Tanzania na Zambia ambapo timu hizo zilitoka sare ya 1-1 huku bao la Serengeti
Boys likifungwa na Miraji Selemani.
Alisema vijana hao leo jioni walitarajiwa kucheza mechi
nyingine wilayani Mbozi dhidi ya Mbozi United huku kesho inatarajiwa kucheza
mechi yake ya tatu jijini Mbeya kwa
kuikabili timu ya daraja la kwanza ya
Mbeya City.
“Kwa mujibu wa Kocha wa timu hiyo, Jakob Michelsen kambi
hiyo inaendelea vizuri, na anatarajia kupata mechi moja ya kirafiki ya
kimataifa kabla ya kucheza mechi ya mashindano na Misri, Oktoba 13 mwaka huu
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam”,alisema Wambura.