MABINGWA wa Afrika Mashariki na Kati, ‘Kagame
Cup’ Yanga, wamezidi kuimarika baada ya wachezaji wake waliokuwa majeruhi akiwemo
kiungo Nurdin Bakari kuanza mazoezi
jana.
Nurdin ambaye alikuwa nje ya dimba kwa
muda mrefu, baada ya kuumia akiwa na timu ya taifa ‘Taifa Stars’, jana
aliungana na wenzake katika mazoezi ya asubuhi kwenye uwanja wa Sekondari ya
Loyola, ikiwa ni maandalizi ya Ligi Kuu Bara itakayoanza Septemba 15.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu,
alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa mbali na Nurdin, viungo Rashid Gumbo na
Athuman Iddi ‘Chuji’ ambao walikuwa na malaria, nao waliungana na wenzao jana
katika mazoezi.
Hata hivyo, Sendeu alisema, kipa wao
namba tatu, Said Mohamed, ambaye naye alikuwa anaugua malaria, hali yake bado
haijatengemaa.
“Naweza kusema kwa kiasi kikubwa kikosi
cha Yanga kipo kamili, baada ya wachezaji waliokuwa wagonjwa kuanza mazoezi…kwa
sasa anayekosekana kundini ni Mganda Hamis Kiiza tu, ambaye yupo kwao
akiitumikia timu ya taifa”, aliongeza Sendeu.
Yanga itaanza ligi hiyo kwa kucheza
ugenini dhidi ya Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye dimba la Sokoine.